Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefuta
umiliki wa mashamba matano yenye jumla ya hekari 14,000 yaliyoshindwa
kuendelezwa na wamiliki wake katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Hatua
hiyo imechukuliwa leo na Rais Magufuli wakati akiwahutubia wananchi wa
Wilaya hiyo alipokuwa anapita kuelekea Tanga kwa ajili ya shughuli ya
uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bomba la
kusafirishia mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga,Tanzania.
Rais
amefuta umiliki huo baada ya baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo
waliopewa mashamba hayo kwa ajili ya kuwekeza katika miradi mbalimbali
ya kilimo ambacho kingeiingizia Serikali mapato, kuyaacha maeneo hayo
bila kufanya uwekezaji tarajiwa.
“Tayari nimeshafuta umiliki wa
mashamba matano yaliyokuwa yamechukuliwa bila kuendelezwa, nimeyarudisha
kwa uongozi wa Mkoa ili wayapange maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za
Serikali pamoja na kuyagawa kwa wananchi. Nasisitiza wananchi wagaiwe
mashamba hayo bure,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli
ameongeza kuwa ardhi ya mkoa wa Tanga haikupangwa kwa ajili ya
wawekezaji bali ni ardhi kwa ajili ya wananchi wote hivyo wana haki ya
kupewa bure ardhi hiyo iliyoshindwa kuendelezwa.
Katika safari
hiyo ya kuelekea Tanga mabapo alisimama maeneo mbalimbali kuwahutubia
wananchi, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi
Robert Gabriel kwa kutumia vizuri fedha za Serikali kuhamasisha vikundi
vya wananchi kujenga madarasa kwa gharama ndogo na kuwataka viongozi
wengine kuiga mfano wake.
Alipopewa nafasi ya kuwasalimia
wananchi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu alisema kuwa utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais
Magufuli unaonesha wazi
dhamira yake ya kutaka kuifanya Tanzania
kuwa mpya hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha hamkatishi tamaa
Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii.
“Tunampongeza Rais
Magufuli kwa juhudi zake za kuibadilisha Tanzania, katika bajeti ya
sekta ya afya ya mwaka huu, tumepewa shilingi milioni 650 kwa ajili ya
kuimarisha kituo cha afya cha Mkuzi, kikubwa ninaomba mtusaidie kuwaibua
wanaouza dawa za Serikali ili tukomeshe tabia hii,” alisisitiza Waziri
Ummy.
Baadhi ya maeneo ambayo Rais alisimama kuongea na wananchi
wakati akielekea Tanga ni pamoja na Mkata, Michungwani, Hale, Muheza na
Mkanyageni.
Rais Magufuli pamoja na Rais Yoweri Kaguta Museveni
wa Uganda wanatarajiwa kuweka Jiwe la Msingi katika mradi mkubwa wa
ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga,
Tanzania. Jiwe hilo la msingi litawekwa eneo la Chongoleani lililopo
Barabara ya Horohoro kuelekea Mombasa nje kidogo ya jiji la Tanga.
Home »
» RAIS MAGUFULI AFUTA UMILIKI WA MASHAMBA MKOANI TANGA
0 comments:
Post a Comment