Na Mwandishi Wetu- Tanga.
Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amekemea
vikali baadhi ya tabia ya viongozi wa timu zinazoshiriki michezo
mbalimbali kutumia wachezaji wasiostahili kutumika katika mashindano
husika.
Ameyasema
hayo wakati akizindua mashindano ya michezo mbalimbali yanayoandaliwa
na Shirikisho la Michezo ya mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMMUTA)
yanayoendelea Jijini Tanga ambayo yameshirikisha timu mbalimbali kutoka
mashirika ya Umma na Binafsi Tanzania.
Mhe.
Nnauye amewataka viongozi wa SHIMMUTA kufanya uhakiki upya wa wachezaji
wa timu shiriki ili kuondoa lawama zinazoweza kutokea na kupata mshindi
anayestahili kwa kufata Sheria na taratibu zote za mashindano.
“Nawaomba
viongozi muangalie na kupitia upya wachezaji wa timu shiriki ili kusiwe
na zengwe lolote katika mashindano haya na mshindi katika kila mchezo
apatikane kihalali” alisisitiza Mhe. Nnauye.
Aidha ametoa wito kwa mashirika
kutenga muda na fedha ili kuwezesha timu zao kushiriki katika michezo
ikiwa ni moja ya kujenga mshikamano na amani kwa watanzania na pia
kujenga afya ya mwili na akili.
Mashindano
ya SHIMMUTA yameshirikisha mashirika ya Umma na Binafsi katika michezo
12 ikiwemo Mpira wa Miguu(Football), Mpira wa Pete(Netball),kuvuta
kamba, Riadha, Mchezo wa vishale(Darts),Mchezo wa Pooltable, mchezo wa
bao, Karata,kukimbia na magunia.
0 comments:
Post a Comment