WAKATI mchakato wa kujenga bomba kubwa la mafuta duniani katika ya
Hoima, Uganda na kijiji cha Chongoleani, nje kidogo ya Jiji la Tanga,
Tanzania ukiwa mbioni, imeelezwa kuwa, kampuni moja ya usafi rishaji ya
Tanzania itaajiri zaidi ya madereva 1,500 kwa ajili ya kazi za mradi huo
kuanzia Juni, mwakani.
Hayo yameelezwa na Harshil Davda, Ofisa Usafirishaji wa Kampuni ya
Simba Logistics inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Tanzania,
Azim Dewji. Davda aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam,
wakati wa kusainiwa kwa makubaliano ya kufanya kazi pamoja baina ya
Chama cha Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS)
na wenzao wa Uganda (AUGOS).
Alisema wapo tayari kuanza kazi na pia wananunua magari zaidi kwa
kuwa mradi unahitaji magari yenye uwezo wa kufanya kazi kwa uhakika na
kwamba yanahitajika kati ya magari 1,000 na 1,500.
Kwa sasa, Simba Logistics ina malori zaidi ya 300 yanayofanya kazi
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, yakisafirisha mafuta na bidhaa
nyingine. Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa AUGOS, Emmanuel Mugarura
alisisitiza mshikamano na ushirikiano wa kweli baina ya nchi hizo, ili
wafanye kazi kwa ubora hivyo kujitengenezea mazingira mazuri ya
kuaminiwa na kupewa kazi zaidi, badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na
kampuni na raia kutoka China, Ulaya au Marekani.
“Tuitumie faida hii kuunganisha nguvu. Lazima tuione faida ya kuwa na
ushirikiano wa Afrika Mashariki,” alisema Mugarura. Mradi wa bomba hilo
unaotarajiwa kukamilika mwaka 2020, unatarajiwa kuwa na urefu wa
kilometa 1,445 kati ya hizo zikitambaa katika ardhi ya Tanzania ambako
itapita katika mikoa minane yenye wilaya 24 na vijiji 184.
Tanzania litapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu,Tabora,
Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Nchini Uganda, litaanzia Ziwa Albert
(Hoima) kwa umbali wa kilometa 296 mpaka mpakani mwa Tanzania.
Wakati wa uzinduzi wa ujenzi huo kijijini Chongoleani, ilielezwa
kuwa, bomba hilo litavutia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
viwanda pamoja na ajira 11,000 za moja kwa moja na vibarua takribani
30,000.
HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment