LEO, Rais John Magufuli na mwenzake wa Uganda, Rais Yoweri Museveni,
watafanya kitendo cha kihistoria kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa
bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania.
Jiwe hilo litawekwa katika Kata ya Chongoleani, takribani umbali wa
kilometa 25 kutoka Tanga Mjini ambako ndiko yatajengwa matangi ya
kuhifadhia mafuta hayo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 500 pamoja na
bandari itakayotumiwa na meli za kusafirisha mafuta hayo kwenda
ughaibuni. Katika kuonesha utayari wa kuandikwa kwa historia hiyo, jana
Rais Museveni aliwasili Uwanja wa Ndege wa Tanga majira ya saa 12:35
jioni akiambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kupokewa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wengine waliompokea Rais Museveni ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine
Shigela, Naibu Waziri wa Madini, Medani Kalemani, Waziri wa Afya, Ustawi
wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na viongozi wengine.
Baada ya kuwasili, alikagua gwaride la heshima lililotayarishwa kwa
ajili yake kisha akasimama kwa muda kuburudika na ngoma ya Msanje
iliyokuwa ikitumbuizwa na akina mama.
Ngoma hiyo kwa kawaida ni ya Kabila la Wadigo ambapo mapema Waziri wa
Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alionesha
ufundi wake katika kuicheza na hata kupiga ngoma hiyo. Waziri Mwalimu
anayeambatana na Rais Magufuli katika ziara ya siku tano mkoani Tanga ni
mwenyeji wa mkoa huo. Tangu saa nane mchana uwanja huo ulifurika mamia
ya wananchi ambao hawakuonekana kuchoka kumsubiri mgeni wao.
Mambo 20 muhimu Timu ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambayo
imekuwa mkoani Tanga kwa takribani wiki sasa na kuwahoji watu
mbalimbali, maofisa wa serikali na Mkuu wa Mkoa, Shigela imegundua
kwamba kuna mambo takribani 20 muhimu yanayolihusu bomba hilo ambayo
Watanzania wanapaswa kuyafahamu. Mosi, bomba hilo litakuwa na urefu wa
kilometa 1,445, karibu mara tatu ya bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar
es Salaam lenye urefu wa kilometa 534.
Pili, uwekezaji wake unategemewa kugharimu Dola za Marekani bilioni
3.5 (zaidi ya Sh trilioni 7) wakati lile la Mtwara liligharimu dola
bilioni 1.2 (Sh trilioni 2.5). Endapo kampuni ya Acacia, kwa mfano,
inayodaiwa Dola za Marekani takribani bilioni 190 (karibu Sh trilioni
400) na Tanzania, hata ikikubali kuilipa Tanzania dola bilioni 100 tu
(Sh trilioni 210), mradi huo mkubwa unaweza kugharimiwa na fedha hizo
bila kuhitaji mikopo ya mabenki.
Tatu, bomba hilo litakuwa na kipenyo cha nchi 24 na hiyo ni kulingana
na aina ya mafuta yaliyogunduliwa Uganda ambayo ni mazito na yenye
kawaida ya kunata. Kwa jinsi hiyo yatakuwa yanasafirishwa kwa njia ya
kupashwa moto. Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar lina kipenyo cha
nchi 36. Nne, hili ni bomba la kwanza kwa urefu duniani kwa mafuta
yanayosafirishwa kwa kupashwa joto.
Na hivyo njiani kutajengwa vituo takribani 10 vya kupashia joto
mafuta hayo. Mafuta katika bomba la Tanzania na Zambia (Tazama) ni ya
kawaida yasiyohitaji kupashwa moto. Tano, bomba litapita katika mikoa
minane ya Tanzania, wilaya 24 na vijiji 80. Mikoa hiyo ni Kagera, Geita,
Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Sita, mkoa wa
Tanga ambako bomba hili litaishia ndiyo utakaofaidika zaidi, kwani ndiko
kwenye matangi na bandari. Wilaya za mkoa wa Tanga ambako bomba
litapita ni Korogwe, Kilindi, Handeni, Muheza na Tanga yenyewe.
Saba, Chati ya Tanga kama mkoa uliokuwa na neema miaka ya 1970, siyo
tu kwa kilimo bali pia viwanda, inatazamiwa kurejeshwa kupitia bomba
hili. Nane, bomba linatarajiwa kutoa ajira 10,000 ndani ya kipindi cha
miaka mitatu ya utafiti, upimaji na ujenzi na ajira 1,000 za kuendelea.
Tisa; karibu kila sekta itafaidika na bomba hilo kama vile makampuni ya
usafirishaji, makampuni ya ulinzi, taasisi za kifedha, huduma za kiafya,
kampuni za chakula na mahoteli, makampuni ya wataalamu (wanasheria,
wahasibu, wahandisi, wataalamu elekezi na kadhalika), wakulima,
wafugaji, wavuvi hadi mama lishe na bodaboda.
Kumi, bomba litahamasisha ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli,
uwanja wa ndege na bandari. Katika eneo la mradi, kilometa 200 mpya
zitajengwa na 150 kuboreshwa. Kumi na moja, kupitia kanuni ya wajibu wa
kampuni zinazoendesha miradi kutoa huduma za kijamii, maeneo mengi
ambayo bomba litapita watapata huduma za umeme, maji, shule, barabara na
kadhalika.
Kumi na mbili, kwa kutumia uzoefu wa Mtwara, bomba litapita huku
likiepuka maeneo yenye shughuli za binadamu kadri inavyowezekana na
hivyo kupunguza migogoro. Kumi na tatu, mradi unajengwa kwa haraka na
unatazamiwa kuchukua miezi 24, sawa na miaka miwili. Zabuni za ujenzi
zinatazamiwa kutangazwa mwishoni mwa mwaka huu na hivyo ujenzi wa bomba
utaanza katikati ya 2018 na kukamilika katikati ya mwaka 2020.
Kumi na nne, mradi unatazamiwa kudumu kwa miaka 25 hadi 30. Kumi na
tano, mafuta yaliyogunduliwa Uganda ni mapipa bilioni 6. Mapipa
yatakayokuwa yanasafirishwa kwa siku kupitia bomba linalozinduliwa leo
ni 216,000 kwa siku. Uganda inatazamiwa pia kujenga nchini mwake kiwanda
cha kusafisha mapipa 60,000 ya mafuta kwa siku.
Kumi na sita, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) ndilo
linalowakilisha Serikali katika mradi huo unaoendeshwa kwa ubia baina ya
serikali za Tanzania na Uganda kwa upande mmoja na makampuni binafsi
kwa upande mwingine. Kumi na saba, mikataba zaidi itaendelea kufanyika
ili kuona kila mbia anamiliki hisa kiasi gani katika mradi huo.
Baada ya mikataba ya nchi na wawekezaji kumalizika, wanahisa wataunda
kampuni ya kuendesha mradi huo. Kumi na nane, kukamilika kwa njia ya
bomba hilo kutahamasisha zaidi tafiti za mafuta na gesi katika maeneo
(vitalu) ambayo yalionekana ya pembezoni. Kadhalika itakuwa rahisi kwa
Tanzania sasa kutumia njia hiyo ya bomba (mkuza) kujenga bomba lingine
pembeni kusafirishia gesi yake kutoka Mtwara hadi mikoa ya kati,
Kaskazini, Kanda ya Ziwa hadi nje ya nchi.
Kumi na tisa, muda wa kuchangamkia fursa za bomba la mafuta kwa
Watanzania ni sasa. Ishirini, Agosti 17 mwaka huu, siku 12 kuanzia leo,
kutakuwa na Jukwaa la Biashara hapa Tanga lililoandaliwa na Kampuni ya
Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na mkoa wa Tanga, ambalo
litasaidia kwa kiwango kikubwa kutangaza fursa zinazopatikana Tanga na
zitakazoletwa na bomba.
Jukwaa litasaidia pia washiriki kujua namna rahisi ya kuziendea fursa
hizo. TSN ambao ni wachapishaji wa magazeti ya HabariLeo, Daily News na
SpotiLeo wameshaandaa majukwaa ya aina hiyo katika mikoa ya Simiyu na
Mwanza na kuleta mafanikio makubwa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment