Imeandikwa na Anna Makange, Tanga
RAIS John Magufuli amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini
kuhakikisha wanasimamia na kutumia vema fedha za maendeleo ili
kuiwezesha serikali kufikia lengo ililokusudia kwa wananchi.
Aliwataka madiwani katika halmashauri kuacha mara moja tabia ya
kushinikiza walipwe posho zao kwa kubadili matumizi ya fedha za
maendeleo zikiwemo za ujenzi wa barabara. Alitoa agizo hilo juzi jioni
wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Muheza katika mkutano wa
hadhara uliofanyika Mkanyageni na kupongezwa na Mbunge wa Muheza, Balozi
Adadi Rajabu baada ya Serikali kupeleka Sh milioni 500 ili
kujenga barabara ndani ya halmashauri.
“Tumieni vizuri hizo fedha mlizopokea kutoka kwenye mfuko wa barabara
kujenga, nakumbuka wakati wa kampeni yangu mwaka 2015 nilitoa ahadi ya
kuwajengea kilometa tatu za kiwango cha lami, hivyo nawaagiza muanze
kutumia Shilingi milioni 500 hizo kwa kujenga kilometa moja.
“Naomba mkurugenzi unielewe, katika fedha hizi zinazotoka kwenye
mfuko wa barabara, siyo za kuwalipa posho madiwani, bali nataka zitumike
tu kwa kazi ya kujenga barabara za lami katika mji wa Muheza, na agizo
hili liwafi kie wakurugenzi na madiwani wote Tanzania kwamba fedha za
mfuko wa barabara zisitumike kufanya shughuli nyingine yoyote,” aliagiza
Rais Magufuli.
Akizungumzia barabara ya Muheza mpaka Amani yenye urefu wa kilometa
40, Rais Magufuli alisema katika bajeti ya mwaka huu tayari Serikali
imepeleka kiasi cha Sh bilioni tatu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
barabara hiyo kwa urefu wa kilometa 10.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment