Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi
amesimamisha umiliki wa mwekezaji wa mashamba ya katani yanayomilikiwa
na kampuni ya Le-Mash Enterprises Limited yaliyopo kata ya Mnazi
wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Waziri
Lukuvi amefikia uamuzi huo baada ya wakazi wa eneo hilo kuzuia msafara
wake na kupata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi hao na viongozi wa
Halmashauri ya wilaya ya Lushoto wakimlalamikia Waziri kuhusu mashamba
matatu ya Mnazi yaliyotelekezwa na mmiliki wa mashamba hayo bila
kuendelezwa na kusababisha migogoro kwa awakazi wa Mnazi.
Baada
ya kupokea malalamiko hao Waziri Lukuvi aliamua kutembelea mashamba
hayo na kuyakagua ili kujionea hali halisi na kuwasikiliza wananchi
ambao wamekuwa wanakabiliwa na mgogoro huu kwa miaka mingi.
Baada
ya kutembelea na kujiridhisha Waziri Lukuvi amesema kwamba shamba hilo
linastahili kufutwa kama ilivyopendekezwa na ofisi ya Mkoa wa Tanga na
ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini kwa kuwa mmiliki
ameshindwa kuwa na sifa za umiliki kwa kuwa hajalipa kodi ya ardhi tangu
mwaka 2004, hajalipa wafanyakazi wake kwa muda mrefu, miundombinu yake
na mazingira ya kazi hayaridhishi na ameshindwa kuliendeleza shamba hilo
tangu akabidhiwe mwaka 1997 kwa kurithi mashine na mitambo ileile ya
mkoloni ya mwaka 1937.
Aidha,
katika ziara hii Waziri Lukuvi amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.
Martin Shigela na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joel Bendera ili kutatua
migogoro ya mipaka iliopo kati ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara na
Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya
kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu ambao umesababisha uvunjifu wa amani.
Waziri
Lukuvi anatekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe. Khassim Majaliwa ambae
alimuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi kutatua mgogoro huu uliodumu kwa miaka mingi kati ya Wilaya hizo
mbili pindi alipofanya ziara yake mkoani Tanga.
Mnamo
tarehe 18 Januari, 2017 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara
Wilayani Kilindi katika Kijiji cha Mafisa na kuzungumza na wanachi
Kijijini hapo kuhusiana na mgogoro huo na kutoa maagizo kwa viongozi wa
kuchaguliwa kuacha kutumia nafasi zao vibaya kuongoza kwa mihemko au
ushabiki kwa kuwa kufanya hivyo kunapelekea wananchi kufuata ushabiki na
kuvunja sheria zilizopo.
Ili
kutekeleza agizo hili wakuu wa mikoa hii miwili wakiongozwa na Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi wamekutana
ikiwa ni muendelezo wa vikao vya kulitafutia ufumbuzi suala hili.
0 comments:
Post a Comment