Home » » MHADHIRI ALISHWA DAWA ZA KULEVYA, AIBIWA KILA KITU

MHADHIRI ALISHWA DAWA ZA KULEVYA, AIBIWA KILA KITU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), Mchungaji Dk Msafiri Mbilu amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga ya Bombo akiwa mahututi baada ya kula keki inayohofiwa kuwa ilikuwa na dawa za kulevya.
Dk Mbilu amepatwa na mkasa huo wakati akiwa kwenye basi akitokea Jijini Dar es salaam kuelekea Tanga.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba ni kuwa mchungaji huyo amebainika kupoteza fahamu baada ya basi hilo kuwasili jijini Tanga na kushindwa kushuka.
Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Bombo, mdogo wa mchungaji huyo, Frank Mbilu amesema amepigiwa simu kwamba kaka yake amelishwa dawa za kulevya na amechukuliwa na askari kukimbizwa hospitalini hapo.
“Nimepigiwa simu nije Bombo, kaka yangu amepoteza fahamu, nilipowasili nilikuta hajitambui, ameibiwa kila kitu kilichokuwa mfukoni kuanzia fedha hadi simu hakuwa nayo,”amesema Frank.
Kamanda Wakulyamba amesema wamepata taarifa kutoka kwa kondakta wa basi ambalo alisafiri nalo ambaye alishtuka alipoona abiria wake hateremki wala hatikisiki mahala alipokuwa amekaa.
“Tumemchukua na kumkimbiza Hospitali ya Bombo kwa matibabu, alikuwa amepoteza fahamu, tunasubiri taarifa ya kitaalamu kutoka kwa madaktari ili kujua ni aina gani ya dawa aliyokula kiongozi huyo,” amesema Wakulyamba.
Kamanda huyo amesema uchunguzi zaidi unafanyika lakini taarifa za awali zinaonyesha kiongozi huyo alikuwa amekula keki na kwamba abiria aliyekuwa ameketi kiti cha jirani yake aliteremkia kituo cha mabasi cha Muheza.
“Tunaendelea kuchunguza kujua aliyempa dawa hizi ni nani na kama ilikuwa imetiwa kwenye keki aliyokula na aliyepora simu na fedha…tuna uhakika kuwa tutamkamata mara moja,” amesema Wakulyamba.

Chanzo Mwananchi



0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa