Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angella Kairuki, amewataka watendaji wa taasisi za
serikali kuwashirikisha watumishi katika masuala mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha wanapata nyaraka mbalimbali zinazotolewa na
serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Waziri Kairuki aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa
mkoa wa Tanga katika kikao kazi na watumishi hao kilichofanyika leo
katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. Kairuki
alisema ni vema watumishi wakashirikishwa katika nyaraka hizo muhimu ili
waweze kujua nini kinaendelea katika serikali yao wakiwa kama watumishi
wa umma.
“Nyaraka hizi zimetengenezwa kwa ajili yao hivyo kukaa kimya bila
kuwashirikisha si sawa, kwani nao wanapaswa kujua ili waweze kutekeleza
majukumu yao ipasavyo,” Kairuki aliongeza.
Alisema kumekuwa na mabadiliko mengi katika miundo, lakini watumishi
hawafahamu kwa sababu hawashirikishwi. Aidha, Kairuki aliwataka
watendaji hao kutenga muda angalau mara moja kwa mwezi ili kusikiliza
malalamiko na kero za watumishi.
“Watumishi wengi wamekuwa wakinyanyasika sana lakini wanashindwa pa
kusemea, hivyo ni vema tukatenga muda wa kusikiliza wanakumbwa na
changamoto zipi,” aliongeza.
Aliongeza kuwa kusikiliza kero za watumishi mara kwa mara kutasaidia
kupunguza malalamiko mengi na watumishi kufanya kazi kwa bidii hivyo
kuongeza pato la taifa.
Ziara yake mkoani humu ni mwendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa
kukutana na watumishi katika mikoa mbalimbali nchini kusikiliza kero na
malalamiko ili kuweza kuyafanyia kazi. Kabla ya kukutana na watumishi
mkoani humu, alikutana na watumishi wa mikoa ya Singida, Dodoma,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment