Home » » Wasafiri wamshitukia mchangishaji wa mchango wa Msikiti

Wasafiri wamshitukia mchangishaji wa mchango wa Msikiti


Na Bryceson Mathias, Korogwe
 

WASAFIRI waliokuwa kwenye gari dogo la abiria linalofanya safari zake kati ya Lushoto na Tanga wamemshitukia mmoja wa ma-ustadhi, anayepanda na kushuka kila basi akichangisha na kukusanya fedha kwa umbali kadhaa, akidai fedha hizo ni za ujenzi wa Msikiti wa Handeni.

 
Ustadhi huyo (pichani na risiti feki), ambaye basi likisimama huingia na kutoa salamu ya Kiislamu, akijinadi anachangisha fedha za Msikiti wa Handeni, jana alishitukiwa baada ya mwandishi wa habari hizi kumhoji maswali kuhusu uchangiaji huo na kuanza kubabaika.

“Msikiti mnaouchangia uko kwenye hatua ya sakafu, na msiwe na hofu, nina kitabu cha risiti, hivyo hakuna udanganyifu wowote unaofanywa, kila anayechangia atapata risiti yake,” alisema baada ya mwandishi wa habari hizi kutaka moja ya risiti alizotoa aichunguze uhalali wake.

Ingawa ustadhi huyo alijitahidi kuzuia risiti isitazamwe na mwandishi ambaye hakumtabua, mwandishi alijitahidi kwa kila mbinu kuipiga picha risiti hiyo, akiwemo yeye mwenye, akiwa na kitabu hicho kwapani karibu na Kituo cha Polisi cha Segera, ila alijitahidi kuuficha uso wake.

Mashuhuda ambao humuona kila siku walidai: 

“Ustadhi huyo huwa anapandia basi stendi ya njia panda ya Handeni – Korogwe, ambapo huchangisha hadi anapofika Segera; baada ya hapo hushuka na kuingia katika mabasi ya Dar es Salaam, ambapo akifika eneo la Menzani hushuka na kurejea na mabasi ya Tanga, Moshi na Arusha akichangisha.

Mmoja wa mawakala wa mabasi ya Simba Mtoto Segera, alisema hata wao (mawakala na watu wengine), wamekuwa wakimuona akipanda na kushuka akikusanya fedha hizo kila siku tangu asubuhi hadi jioni, lakini wamekuwa wakiona kama ni jambo la kawaida na hawajajihoji.

Siku hizi kumezuka mtindo kwenye mabasi ambapo wameibuka wahubiri wanaoingia kwenye mabasi wakidai wanamtangaza Mungu, baadaye huwaomba wasafiri sadaka kwa waliyosema, na hakuna mtu anayewashitukia kuwa wametumwa na nani makanisani mwao kufanya hivyo.

“Ni vizuri serikali ikawa na umakini wa mambo haya yanayofanyika kwenye mabasi, kwa sababu kumekuwa na usumbufu mkubwa, maana wengine wanaingia na mizigo mikubwa ya vinywaji, vitafunwa au kuuza dawa.

“Tunawataka wamiliki wa mabasi na serikali wakomeshe hali hiyo, maana punde watu hao wakishuka na mizigo ya bidhaa wanazouza ghafla abiria huanza kulalamika wameibiwa,” alisema mama mmoja msafiri, aliyeomba asitajwe jina.
Na Habari Mseto Blog

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa