Ikipitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.wa unatukio lolote au jambo lolote tuma ku
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga.
Watu 103 wamepoteza maisha na wengine 138 kujeruhiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Machi 11 hadi Aprili 12 mwaka huu, kutokana na ajali za barabarani.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu baadhi ya matukio ya ajali yaliyotokea hivi karibuni.
Kamanda Mpinga alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi sasa, zimetokea ajali nane, vifo 103 na majeruhi 138.
Alisema kwa kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi kumetokea vifo vya watu 866 na majeruhi 2,370 kutokana na ajali hizo.
“Kuanzia Januari zimetokea ajali 823 vifo 273 majeruhi 876, mwezi Februari zimetokea ajali 641, vifo 236 majeruhi 726 na Machi zimetokea ajali 652, vifo 357 na majeruhi 761,” alisema Mpinga.
Alisema baadhi ya matukio makubwa ya ajali hizo ni miongoni mwa ajali mbaya ambazo zilitokea Marchi 11, mwaka huu katika kijiji cha Changarawe, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa iliyohusisha magari mawili likiwamo basi na lori la mizigo na kuua watu 50 na majeruhi 22.
Alisema Machi 19, mwaka huu eneo la Mikumi Mbugani mkoani Morogoro, ilitokea ajali iliyohusisha gari aina ya Tata na basi la abiria na kusababisha vifo saba na majeruhi 17.
Aliongeza kuwa Machi 17, mwaka huu mkoani Morogoro, eneo la Mikumi Mbugani ilitokea ajali kati ya basi na lori aina ya Fuso ambayo ilisababisha vifo vya watu wawili na majeruhi nane.
Alisema Aprili Mosi, mwaka huu mkoani Morogoro, ilitokea ajali na kusababisha vifo vinne, majeruhi 47 na Aprili 3, mwaka huu mkoani Morogoro Makunganya ilitokea ajali iliyohusisha mashabiki wa Klabu ya soka ya Simba na kusababisha vifo saba na majeruhi 22.
Alisema Aprili 9, mwaka huu mkoani Tanga katika eneo la Mkata ilitokea ajali iliyosababisha vifo 10 na majeruhi 12.
Aliongeza kuwa Aprili 10, mwaka huu mkoani Dodoma, ilitokea ajali iliyosababisha vifo vinne na Aprili 12 ilitokea ajali Mkoa wa Morogoro eneo la milima ya Ivori na kusababisha vifo 19 na majeruhi 10.
Alitoa wito kwa wamiliki wa mabasi kuwahamasisha madereva kupunguza mwendo kasi.
Pia, Mpinga alisema madereva watakaosababisha ajali watafutiwa leseni na aliwataka wamiliki kuajiri madereva wawili katika safari ndefu ili kupunguza ajali za barabarani.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment