Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana gesi na mafuta katika miamba tabaka iliopo eneo la Gombero Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga baada ya utafiti wa awali kuonyesha dalili nzuri.
Kaimu Mkuregenzi wa shirika hilo, Dk. Emma Msaky, aliyasema hayo jana alipotembelea eneo la mradi kwa lengo la kukagua shughuli za uchorongaji wa mashimo madogo 10 yatakayotumika kuchukua sampuli za miamba tabaka ili kujua ubora wake.
Dk. Msaky alisema kuwa utafiti ulianza mwaka 2010 katika vijiji vya Nairobi, Pangarawe na Jirihini ambapo ndipo miamba tabaka ilipo na uwezekano wa kupatikana kwa nishati hizo ni mkubwa.
“Mradi huu unatarajia kumaliaka mwaka 2019 na utagharimu zaidi ya Shilingi milioni 300 ambazo asilimia 100 zimetoka kwenye mfuko wa maendeleo wa shirika na hata watafiti ni wetu,” alisema. Aliongeza: "Malengo makuu ya mradi huo ni kuendelea kuyaainisha maeneo ya utafutaji wa mafuta na gesi ili kujua uwapo wa miamba ya uzalishaji."
Naye Mratibu wa mradi, Frank Mayagilo, alifafanua kuwa mradi huo umegawanyika sehemu tatu ambazo ni utafiti wa kuainisha maeneo husika ambayo ilishafanyika, kuchoronga mashimo madogo na uchimbaji wa visima virefu, kazi ambayo itafanyika baadaye.
Alisema gesi inayopatikana katika miamba tabaka hujulikana kama `shale gasi' ambayo tofauti yake na inayochimbwa kwenye kina cha maji hutumia muda mfupi takribani miaka mitatu.
“Tukifanikiwa kupata shale gasi itasaidia mambo mengi ikiwamo ajira, makusanyo ya kodi, kuongeza upatikanai wa nishati ya umeme na bei ya gesi itashuka kwani uchimbaji wake ni wa muda mfupi,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Jirihini, Jumaa Kasidina, alishukuru mradi unaondeshwa na wazawa wataalam kutoka ndani kwamba utakuwa mkombozi wa maisha yao.
Naye Ofisa Mazingira kutoka TPDC, Johannes Kakoki, alisema kabla ya mradi huo, walifanya utafiti wa kimazingira kuhakikisha mradi huo hauathiri viumbe hai vilivyopo kwenye eneo hilo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment