Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Aidha, Kinana amewataka viongozi wasijisahau na kuwatahadharisha kwamba atakayejisahau ama kuwa `bize' na shughuli zake binafsi, basi ajiondoe mapema na kuwapisha wengine kabla ya kutimiliwa.
Alisema watu wa namna hiyo watakuwa kikwazo kwa Chama kushindwa kuwatumikia wananchi.
Kinana aliyasema hayo wakati akiwahutubia wakazi wa Jiji la Tanga katika mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye uwanja wa Tangamano jana.
Alieleza kuwa viongozi wenye mawazo ya kuimba nyimbo kwa kuisifu serikali hata kama hakuna sababu ya msingi, hawana uwezo wa kuikosoa, jambo alilosema kuwa watu hao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa chama hicho kushindwa kuwatumikia wananchi ambao ndiyo matajiri wao.
Alisisitiza kuwa kiongozi anayefikiria kuiimbia nyimbo nzuri serikali kwa sasa, hatoshi kwa kuwa siyo kazi ya chama hicho na kuwataka wasimamie utendaji kazi wa serikali ikiwamo kukagua miradi na kuhoji pale inapobidi endapo kuna utata.
“Kuleni firigisi, lakini chapeni kazi, nendeni vijijini mkasikilize kero za wananchi, siyo nyimbo, nyimbo pekee hazitoshi na wananchi hawana shida nazo hizo...wanataka maendeleo na ufumbuzi wa kero zao,” alisema Kinana.
Aidha, alisema tatizo la uadilifu na uaminifu kwa viongozi ni kubwa na kwamba limefikia wakati sasa wananchi kuitilia shaka CCM.
Alisema kuwa ufike wakati kila mmoja ashuke chini kuwatumikia watu ili kujenga imani kwa jamii.
Kinana alisema uongozi wa sasa ni mgumu na kuwataka wale wanaodhani kuwa ni burdani, sherehe na starehe, wamepotea na kuwataka wakatafute kazi nyingine za kufanya kwa kuwa huku ni utumwa na kutumikishwa na si vinginevyo.
Kwa upande wa uchaguzi wa serikali za mitaa, Kinana alielezea mafanikio makubwa yaliyokipata chama hicho.
Hata hivyo, alishauri kufanyika kwa tathmini ya matokeo hayo na kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza ili zisijirudie kwenye uchaguzi ujao wa madiwani, wabunge na Rais.
Kinana alisema CCM imepata ushindi katika maeneo mengi nchini katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Alikejeli kauli za watu wanaodai CCM imefanya vibaya katika uchaguzi huo na kusema ni hizo ni ndoto za mchana.
"Hao ni sawa na fisi mwenye matumaini na mkono wa mwanadamu anayetembea akidhani utadondoka apate lishe," alisema Kinana.
SOURCE:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment