Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Zimesalia siku chache kabla ya kuingia mwezi mwingine wa Novemba. Ni mwezi mchungu kwa watendaji wa wilaya kupitia halmashauri mbalimbali waliopewa hadi mwezi huo kuhakikisha wanajenga maabara za masomo ya sayansi. Rais Jakaya Kikwete aliagiza kujengwa maabara za shule katika maeneo yao na kuwataka kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inakamilika mapema.
Akiwa katika mikutano ya hadhara katika wilaya za Lushoto na Kilindi mkoani Tangakatika ziara yake hivi karibuni, alisema anataka ifikapo Novemba mwaka huu aone vyumba vya maabara vimekamilika.
Mwaka 2012, Rais alitoa agizo kwa watendaji hao akawakumbusha tena juzi kwa kuwaambia, “Tulipeana miaka miwili....“Nilishatoa maagizo kama miezi michache iliyopita kuwa kila mkuu wa wilaya ahakikishe anajenga maabara katika shule zake za kata sasa watu wanafikiri ni mchezo wataniona Novemba kama nilikuwa natania,” alisema Rais Kikwete.
Rais pia aliongeza kusema kuwa anaridhishwa na upanuzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini lakini alisisitiza umuhimu wa kutilia mkazo katika eneo la ubora wa elimu, upungufu wa waalimu na upatikanaji wa vitabu na nyumba za waalimu.
Ninapongeza hatua hiyo ya Rais Kikwete kuwabana watendaji wake, japokuwa naona kama amri imechelewa mno. Haya mambo yalitakiwa katikati ya muhula wa kwanza wa uongozi wake. Katika miaka mitano, miaka miwili ya kujipanga, lakini miaka mingine minane ni kusimamia utekelezaji wa kila eneo kulingana na mahitaji.
Ninapongeza kwa kuwa nilisikia baadhi ya watendaji kila kona wakizungumza katika vyombo vyahabari, kuwa wanakimbizana na ahadi ya JK. Tena uzuri amekwisha sema kwamba watakaoshindwa kukamilisha ujenzi huo, wataonana Novemba na hakuna msalie mtume.
Haya ndiyo mambo tunayoyataka. Watanzania tumekuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea.
Maabara zijengwe, watengenezwe walimu wa sayansi na masomo mengine ili kuwasaidia wanafunzi kupata uhalisia wa kile wanachojifunza kupitia maabara.
Ukamilishwaji wa maabara hizo, usiwe kuwa jengo pekee, maabara hizo ziendane na upatikanaji wa vifaa vyake timilifu. Ninaungana na hili kwa watakaoshindwa ama iwe ndiyo tiketi yao ya kujitathmini upya au wachunguzwe utendaji kwenye halmashauri zao kama kweli fedha hakuna.
Itashangaza kusikia kuwa halmashauri fulani imeshindwa kujenga maabara za kisasa kwa ukosefu wa fedha, hao watakaoshindwa, wachunguzwe vitabu vyao vya hesabu.
Kumekuwa na ripoti mbaya za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, katika baadhi ya Halmashauri, wilaya na mikoa kuwa watu ‘wanapiga’ hela vibaya hata kushindwa kufanya maendeleo.
Tuanze kuwachunguza huku. Ninakumbuka kuna wakati tulielezwa bungeni kuwa Wakurugenzi Watendaji (DED) wa Halmashauri mbalimbali nchini 73 wamefukuzwa kazi, 78 wanakabiliwa na kesimahakamani, 33 wamesimamishwa na mmoja amestaafishwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri hizo.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment