Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Sasa ni dhahiri kwamba mwelekeo wa nchi yetu umetufikisha mahali
pabaya. Haya tumeyasema, tumeyaandika, wengine tumeyahubiri, lakini
serikali yetu tukufu ya CCM haisikiii.
Mara nyingi kwa watu waliosema hayo, wameonekana
ni ‘maadui nambari wani.’ Ni kitu cha kusikitisha kwa taifa kama hili
ambalo ni changa lakini lenye kubarikiwa na Mwenyezi Mungu.
Waswahili husema, penye miti hakuna wajenzi.’
Siasa za nchi yetu zilianza vyema na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere ambaye anaweza kufananishwa kama ‘Musa’ aliyewatoa Waisraeli
utumwani.
Kazi ya kuleta ukombozi ni kazi ngumu kwa kiongozi
na wanaowangoza, kwani inahitaji ubunifu, upendo, uzalendo, heshima,
utu na uvumilifu mkubwa.
Mwalimu Nyerere alijenga taifa lenye umoja,
heshima, undugu, usawa, upendo, amani na haki, chini ya siasa za ‘Ujamaa
na Kujitegemea’ kama dira yake ikaimarishwa na Azimio la Arusha la
1967.
Mwalimu alijitahidi kufuta utemi na kuwaunganisha
Watanzania wakazungumzia lugha moja ya kindugu. Hata hivyo, baada ya
Mwalimu Nyerere kufariki dunia, viongozi waliofuata walianza kuachana na
misingi mizuri aliyoiasisi. Leo, nchi yetu imegawanyika vipande chini
ya Serikali ya CCM. Chini ya Mwalimu Nyerere, CCM ailikuwa na umoja,
dira, sera nzuri, ilikuwa na upendo.
Ile ya Nyerere ilipendeza, kupendwa na Watanzania
karibu wote. Lakini, CCM ya leo inayounda Serikali ya Tanzania imegeuka
na kuwa kama ‘mnara wa Babeli’ (Mwanzo 11:19). Kwa nini naifananisha CCM
ya leo na mnara huo maarufu? Ni kwa sababu ya hali halisi ya siasa
katika nchi yetu. Waisraeli walipofika katika nchi ya Shinar walifyatua
matofali na kujijengea mji na mnara ili kuichungulia mbingu kwa majivuno
ya kujiona wao sasa ni sawa na Mungu.
Kisha, wakasema ngoja tujitengenezee jina kwa
ajili yetu. Lakini, Mungu aliposhuka kutoka mbinguni alipoona jinsi
walivyojaa majivuno, kiburi, dharau, ulevi wa madaraka akawasambaratisha
kwa kuwachanganya wasisikilizane tena. ( Mwanzo 11:1-9). Na huo ndiyo
ukawa mwisho wao.
CCM ya sasa imekuwa kama mnara wa Babeli, hakuna
umoja, upendo, amani, kuamini, heshima, dira, sera za kujali wanyonge,
kuwatumikia wananchi.
Ndani yake, kuna kejeli, vitisho, kiburi na ubabe.
Kwa nini tuifananishe na Mnara wa Babeli? Askofu Mkuu Zakaria Kakobe wa
Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship alishatoa utabiri kama huo huo,
kwamba CCM itasambaratika, na je, nini kinaendelea kutokea hadi leo hii
na hasa ukitazama kinachojiri kwenye Bunge Maalumu la Katiba huko
Dodoma? CCM inazidi kujikaanga kwa kupanga kila aina ya mizengwe, hila,
fitina, unyanyasaji kwa raia na wapinzani kwa kutumia vyombo vyake.
Je, hii si alama ya kusambaratisha kama mnara wa
Babeli? Mungu wetu ni Mungu wa haki, mtu mwenye fitina na chuki,
hatafika mbali, maandiko yanasema.
Kuendelea kujidanganya kwamba CCM inapendwa na
inakubaliwa na Watanzania wengi ni kuonyesha upofu wa hali ya juu, ulevi
wa madaraka. Matokeo yake ni kulazimisha, kitu ambacho ni alama wazi ya
kushindwa kuendesha nchi kwa kufuata sheria, kanuni na katiba
Bahati mbaya kuna wana- CCM na viongozi wa serikali ambao kwa
makosa ya fikra, kiburi na utamu wa madaraka bado wanajidanganya na
kuamini kuwa chama chao kitadumu milele. Hawa pamoja na mashabiki wao
wapenda madaraka na mafisadi wamejiaminisha katika upotofu wao kuwa
chama hiki kitatawala milele, kitadumu milele na kitaendelea kuwa kama
kilivyo sasa milele na milele!
Hawa ni wale wanaotakiwa kuombewa kwani wana ‘pepo la ulevi wa madaraka’ ambao ni ugonjwa mbaya.
Niseme tu kwamba CCM ni tunda la fikra na kazi ya binadamu; ni chombo kilichoundwa na wanadamu, kinaongozwa na binadamu.
Kwa hiyo, CCM ni chombo kinachoweza kuharibika,
kuvunjika, na mwishowe kinaweza kufa. Vyama vingi vikongwe Afrika kama
vile, Kenya (KANU), Malawi (MCP), Zambia (UNIP) na kadhalika vilikufa.
Busara za kibinadamu zinatuambia,‘ kila kitu kina
mwanzo na mwisho’. Hivyo, CCM lazima itafika mwisho kama siyo leo ni
kesho, na kama siyo kesho, keshokutwa, hii ni kawaida.
Watu wengine wanapokaribia kufa huhangaika na kutapatapa wakijaribu kujiuliza kwa nini mimi, hutafuta mchawi wao ni nani?
Leo, CCM inahangaika kutafuta mchawi wake ni nani
na inapoteza muda mwingi kushughulika na wapinzani, kuwadhibiti badala
ya kujenga sera za kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la
umaskini. Mchawi wa CCM ni wao wenyewe lazima ifike mahali wajitafiti.
Nchi inadai mabadiliko, je wapo tayari kuyaongoza mabadiliko hayo kwa
usalama na umakini?
Saikolojia ya magonjwa ya akili inatufundisha
kwamba dawa pekee ya kupona magonjwa hayo kama ulevi wa dawa na pombe ni
kujikubali kwamba una tatizo, la sivyo utaendelea kusteseka.
Hivyo, ninaposikia mtu anasema kwamba hakuna
ufisadi ndani ya CCM anashangaza. Nikimsikia anayesema ‘CCM ni safi’,
naendelea kumshangaa zaidi, nikisema mwenzetu anazungumzia CCM gani ya
Mwalimu Nyerere au hii ya leo? Pia, ninapowasikia wapiga propaganda wa
CCM wamekazana kuitetea kuwa ni chama safi na kina ‘mafisadi wanne’,
ninafumba macho yangu na kujiuliza ‘hivi ni kweli’ au ni porojo?
Au hii ni alama ya kukata tamaa na alama wazi ya
kugeuka mnara wa Babeli na ulevi wa madaraka. Matukio ya ajabu
tunayoyasikia sasa na kuyashuhudia hivi sasa ndani ya CCM ni alama wazi
kwamba chama hiki kikongwe barani Afrika hakika CCM iko matatani na
hakuna mtu wa kuiokoa. Haiokoleki kwa sababu imegeuka na kuwa kama mnara
wa Babel
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment