Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAULI
iliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga ambaye pia
ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Bw. January
Makamba, akidai Tanzania kwa sasa inahitaji Rais kijana, imeanza kuibua
maswali kwa baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani
Shinyanga.
Katibu Mwenezi wa CCM
Wilaya ya Shinyanga mjini, Bw. Charles Shigino, alisema kauli ya Bw.
Makamba aliyoitoa akiwa nchini Uingereza inaweza kusababisha mgawanyiko
mkubwa ndani ya CCM kwa vile inaonesha ubaguzi wa wazi kwa baadhi ya
wanachama wake. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga jana,
Bw. Shigino alisema yeye binafsi anailaani kauli hiyo ambayo
ameifananisha na siasa za ubaguzi ndani ya chama ili kulibagua kundi
moja la wanachama.
Alisema CCM, imekuwa
ikipinga suala la ubaguzi wa aina yoyote hivyo kauli ya Bw. Makamba
kutaka Rais ajaye mwaka 2015 awe kijana inaweza kusababisha mpasuko
kwani inapingana na Katiba ya CCM.
“Makamba anapaswa
kuelewa kuwa, ujana si kigezo cha kuwa na sifa za kugombea nafasi ya
urais, nafasi hii ni nyeti na mtu anayechaguliwa anapaswa kuwa na
busara, uwezo wa kuongoza nchi bila kuyumba.
“Wapo wazee wenye sifa
hizi kuliko vijana...kauli hii pia inapingana na Katiba ya chama chetu
labda paitishwe Mkutano Mkuu tuweze kufanya mabadiliko ya Katiba
vinginevyo hoja ya ndugu yetu haitakuwa na mashiko kama wazee
watajitokeza kuwania urais,” alisema.
Aliongeza kuwa; “Katiba
ya CCM Ibara ya 14 vifungu vidogo vya (1) hadi (3), vinafafanua wazi
juu ya haki za mwanachama ikiwemo ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi,
hapa haijataja wenye haki hiyo ni vijana tu, inawezekana Makamba,”
alifafanua Shigino.
Alisema ni vizuri Bw.
Makamba akajifunza kutoka kwa wazee waasisi wa taifa hili ambao waliwahi
kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa badala ya kutoa kauli zinazoashiria
mianya ya ubaguzi ndani ya CCM hivyo kuhatarisha mstakabali wa chama
katika chaguzi zijazo.
“CCM ni chama kikongwe
nchini, ndani yake kuna akina mama, wazee na vijana ambao wote wana haki
sawa kwa mujibu wa katiba yetu, mimi sioni tatizo la mgombea urais kwa
tiketi ya CCM atokane na vijana au wazee, wote ni sawa, mradi wawe na
sifa, vigezo vinavyohitajika,” alisema.
Shigino aliviomba vikao
mbalimbali vya uteuzi ndani ya CCM, kuipuuza kauli ya Bw. Makamba na
wajumbe wake wasiwe tayari kuongozwa na matakwa ya watu, bali wazingatie
katiba na kanuni za chama katika uteuzi wao na muhimu kuangalia mtu
gani mwenye uwezo wa kuivusha CCM 2015 bila kujali ni mzee au kijana
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment