Home » » RAIS KIKWETE AANZA ZIARA TANGA

RAIS KIKWETE AANZA ZIARA TANGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete
 
Wakati Rais Jakaya Kikwete akianza ziara ya siku nne kutembelea mkoa wa Tanga leo, Mkuu wa mkoa huo, Chiku Gallawa, amewaagiza wakuu wa wilaya za mkoa huo kusimamia mazao ya  wakulima na kuwadhibiti wafanyabiashara wanao walangua wananchi na kuwadidimiza katika umaskini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Gallawa, aliwahimiza viongozi hao kuhakikisha walanguzi hawapati nafasi ya kuwarubuni wakulima na kuwataka kutoa elimu  ya usalama wa chakula kwa wananchi vijijini ili kuziondolea wilaya hizo aibu ya njaa.

Gallawa ambaye  aliitisha kikao hicho kwa ajili ya kutoa taarifa ya ziara ya Rais, Jakaya Kikwete, inayotarajiwa kuanza leo wilayani Kilindi, alisema pamoja na jitihada zinazofanyika kuhimiza kilimo, wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaowanyonya wakulima mazao yao  hivyo kushindwa kujikwamua kiuchumi na kubaki katika umaskini.

Kuhusu ziara ya Rais Kikwete, Gallawa alisema itakuwa ya siku nne katika wilaya za Kilindi, Lushoto, Mkinga na Pangani, ambapo majumuisho yake yatafanyika Pangani Julai 12, mwaka huu ikiwa ni hitimisho la ziara yake mkoani humo.

Alisema katika ziara hiyo, Rais atahamasisha shughuli za maendeleo, atakagua, kuzindua na kutembelea miradi mbalimbali, ikiwamo kugawa pikipiki kwa watendaji wa kata, mradi wa nyuki Lushoto na uzinduzi wa nyumba za wafanyakazi wilayani Mkinga, huku Pangani akitembelea vikundi vya wajasiriamali.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa, aliwataka wananchi wa Tanga kusaidia suala la ulinzi kwani ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha usalama unakuwapo ili  kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea kama zilivyopangwa.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa