Home » » WANAKIJIJI GARE WAOMBA KATAPILA

WANAKIJIJI GARE WAOMBA KATAPILA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
WANAKIJIJI wa Gare, Kata ya Magoroto wilayani Muheza, Tanga, wameiomba serikali kuwapelekea katapila ili wamalizie ujenzi wa barabara kuu itokayo Amani kuelekea Muheza.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano jana, katibu wa wananchi wapenda maendeleo wa kata hiyo, Andrew Kibuyu, alisema barabara hiyo inatoka Kijiji cha Kwamatinda kuelekea Gare haijakarabatiwa tangu enzi ya ukoloni.
Kibuyu alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo inayowaunganisha na barabara kuu ya Amani-Muheza kutasaidia kumaliza matatizo ya wananchi hao katika shughuli za kijamii ikiwemo kufika hospitali ya wilaya.
“Hivi sasa wakazi wa Gare tunalazimika kuwabeba wagonjwa kwenye machela umbali wa kilometa saba hadi barabara kuu inayotoka Amani kuelekea hospitali Teule… shida zaidi wanapata wajawazito wanapotaka kujifungua.
“Sisi wanakijiji cha Gare tumefanya jitihada ya kujitolea nguvu zetu kwa ajili ya kukarabati barabara hii na tayari tumefikia kilomita 3.5.
“Tumetuma nakala za barua za kuomba msaada kwa Waziri Hawa Ghasia (Tamisemi), Mkuu wa Mkoa Tanga, Chiku Galawa, Ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mbunge wa Muheza Herbert Mntangi na Halmashauri ya Muheza, lengo letu ni kupatiwa katapila hilo,” alisema.
 Chanzo:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa