Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI
imeshauriwa kuanzisha juhudi za makusudi zitakazosaidia kukabiliana na
uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango zinazoingizwa nchini ikiwemo
saruji.
Ushauri huo umetolewa na kampuni ya kuzalisha saruji ya
Tanzania Portland Cement Company (TPCC) wakati wa ziara ya Kamati ya
Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara iliyotembelea kiwanda hicho
mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya TPCC, Pascal
Lesoinne, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Saruji
Afrika Mashariki (EACPA), alisema suala hilo kama halijapatiwa ufumbuzi
litaathiri uhai wa kampuni nyingi nchini na hatimaye kuathiri uchumi kwa
ujumla.
"Kampuni nyingi za Tanzania za uzalishaji saruji
zinakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa saruji itokayo nje hasa
Pakistan," alisema na kuongeza;
"Waingizaji wa saruji toka nje
wanatumia ipasavyo mianya iliyopo katika mfumo wa forodha na uingiaji wa
bidhaa kwa kulipa kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya ushuru wa
forodha, hali ambayo inaigharimu nchi hasara ya zaidi ya sh. bilioni
25," alisema, Lesoinne
Aliongeza kuwa Tanzania haihitaji saruji ya
kutoka nje kutokana na uwepo wa kampuni nyingi zinazozalisha saruji
hivyo zinaweza kufikia mahitaji ya nchi kikamilifu.
Kwa upande
mwingine alisema kutopatikana kwa umeme wa uhakika kumeongeza gharama za
uendeshaji wa kampuni yake. Alitoa mfano kuwa kampuni yake inatumia
zaidi ya dola milioni 2 kwa mwezi ili kuhakikisha umeme mbadala
unapatikana pindi umeme wa TANESCO unapokatika.
"Changamoto kubwa
inayoathiri uzalishaji wetu ni kutokuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa
uhakika hivyo lazima kampuni ihakikishe kuwa wateja wanaendelea kupata
bidhaa zetu kwa wakati wote bila kikwazo," alisema.
Alisema kwa sasa
wanazalisha zaidi ya tani milioni 1.3 za saruji kwa mwaka itaweza
kuzalisha hadi tani milioni 2 kwa mwaka baada ya uzinduzi wa kiwanda
chake kipya Oktoba, mwaka ujao.
Kwa upande wake, Mbuge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila, alieleza wasiwasi kuhusiana na jitihada
zinazochukuliwa na mamlaka husika na kuziomba kufanya uchunguzi sahihi
kujua ukweli wa suala hilo.
"Hili ni suala nyeti sana. Sisi kama
kamati hatuwezi kulifumbia macho kwa kuwa lina athari kwenye maendeleo
ya uchumi wa nchini yetu," alisema Kafulila.
Mkurugenzi wa Viwanda
katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Eliness Sikazwe, alisema Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, tayari ameteua kamati ya
wanachama saba kuchunguza suala hilo na kuongeza kuwa kamati hiyo itatoa
ripoti baada ya uchunguzi kukamilika.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment