Home » » Wavamia shamba la mwekezaji,waua Bwana Shamba

Wavamia shamba la mwekezaji,waua Bwana Shamba

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Costantine Massawe.
 
Bwana Shamba wa shamba la mkonge Kumburu Estate wilayani Muheza, Jeseph Kaduli amefariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wasiofahamika kutokana na mgogoro wa ardhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe (pichani)  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi katika kijiji cha Kwamnyefu wilayani hapa.

Alisema marehemu alikuwa Bwana Shamba katika shamba la mkonge Kumburu Estate ambalo linamilikiwa na mwekezaji Hamisi Kindoroko na kwamba chanzo ni mgogoro wa ardhi kati ya wakulima wadogo na mwekezaji wa shamba hilo.

Hivi karibuni kulitokea mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji huyo wa shamba la mkonge Kumburu na wakulima wadogo katika kijiji cha Kwamnyefu.

Kindoroko alidai kuwa, wakulima wadogo walivamia shamba lake la mkonge ambalo ana hati nalo na kuanza kulima machungwa.

Alisema alitoa taarifa kwa uongozi wa wilaya akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mstaafu Mathew Nasei kuhusiana na mgogoro huo ambaye alifika na kuitisha mkutano kijijini hapo kati ya yeye mwekezaji na wakulima wadogo.

Alisema katika mkutano huo ilionekana kwamba wakulima hao wadogo wamevamia shamba hilo kwa kuwa ana hati halali ya umiliki.

Alisema hata hivyo baada ya mkutano huo, alipeleka katapila na kuanza kulima katika mashamba ya wakulima wadogo, hivyo wakulima hao waliamua kwenda mahakamani kushitaki na hukumu ilitoka kwamba sehemu hiyo yenye mgogoro inamilikiwa na mwekezaji kihalali na karatasi za hukumu zimesambazwa kwa wenyeviti wa vijiji na polisi Muheza.

Hata hivyo, Kindoroko alisema juzi walifika watu wa kupima eneo hilo la ardhi ili kuanza kazi ya kulima mkonge lakini walipoondoka na kubaki Bwana Shamba lilijitokeza kundi la watu na kumvamia kisha kumpiga na kumjeruhi vibaya na kukimbizwa Hospitali Teule Muheza ambako alifariki dunia.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa