Home » » Wakulima wa chai Bumbuli waishauri serikali

Wakulima wa chai Bumbuli waishauri serikali

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wakulima wakiwa katika kikao 
 
Wakulima  wa chai katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli wameishauri serikali kumtafuta mwekezaji mwingine wa kiwanda cha chai ili kuinusuru chai inayoendelea kuharibikia mashambani tangu kufungwa kwa kiwanda cha Mponde miezi minane iliyopita.
Aidha, wakulima hao wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati mgogoro uliopo baina yao na mwekezaji wa kiwanda hicho ili kunusuru uchumi wao na pato la taifa kwa ujumla.

Kiwanda cha Mponde ambacho Umoja wa Wakulima wa Chai Utega wanamiliki asilimia 50 na mwekezaji asilimia 50  kilifungwa baada ya wakulima kugoma kupeleka majani  mabichi  ya  chai yao wakidai mwekezaji huyo anawalangua.

Wakulima hao pia walilalamika kuwa uongozi wa Chama  cha  Wakulima Utega umekuwa sehemu ya mwekezaji huyo na hivyo kuwatelekeza katika masuala muhimu ya kusimamia na kutetea maslahi yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE, wakulima hao walisema tangu kiwanda hicho kifungwe mwaka jana, chai yao inaendelea kuharibikia mashambani na kuwafanya kuwa na hali ngumu kiuchumi.

Mkulima wa chai katika halmashauri hiyo, Rogath Teme alisema wakulima wanachokiomba kwa serikali ni kuwafungulia kiwanda chao ili chai yao isiendelee kuharibika mashambani na kwamba kama serikali haitafanya hivyo watakifungua kiwanda hicho wenyewe kuinusuru chai yao.


Teme alisema baada ya kufikia maamuzi ya kukifunga kiwanda hicho, serikali iliunda tume ambayo baadaye ilipendekeza kuundwa kwa uongozi wa muda katika kiwanda hicho lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika wakati hali zao zinaendelea kuathirika kiuchumi.

"Maamuzi ya kufungwa kwa kiwanda tuliyafanya sisi wakulima na tulifanya hivyo kwa maslahi yetu, sisi maamuzi yetu hatumtaki mwekezaji, tunachotaka ni kumpata mwekezaji mwingine huyu hapa tulipofikia naye panatosha," alisema Tembe.

Naye  Juma  Frana  alieleza  kuwa, kwa kipindi hiki wakulima wa chai Bumbuli inawabidi wapeleke chai yao kwenye kiwanda kidogo cha Dindira na Hekulu wilayani Korogwe na mvua zinaponyesha  usafiri huwa mgumu na hata uwezo wa viwanda hivyo ni mdogo ikilinganishwa na chai wanayozalisha.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Bumbuli, Beatrice  Msomisi alisema tangu kiwanda hicho kilivyoacha kufanya kazi halmashauri hiyo imeathirika kiuchumi kwani kilikuwa tegemeo la wakulima wengi wanaolima chai katika eneo hilo.

Hata hivyo, aliwaomba wakulima kuvuta subra wakati serikali ikiangalia namna ya haraka ya kutatua mgogoro huo ambao umedumu miaka 13  iliyopita kabla ya kufungwa rasmi kwa kiwanda hicho mwaka jana.

Kilimo cha chai ndicho kilimo pekee kinachotegemewa na halmashauri ya Bumbuli kiuchumi na mgogoro huo umepelekea kurudisha nyuma maendeleo ya wakulima wa chai katika halmashauri hiyo.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa