Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM),Stephen Ngonyani.
Kiongozi huyo Stephen Ngonyani, mbunge wa Korogwe Vijijini alisema kutokana na kutojali shida za wananchi wengi maskini baadhi ya Watanzania wamejenga chuki baina ya masikini wa kipato na wale wenye nacho.
Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu alisema wanachama hao wachumia tumbo watakiathiri chama kwa kuwa wamewaacha walalahoi wakiteketea kwa magonjwa na umasikini, huku wao wakiponda raha kwa kula kodi za wavuja jasho.
Mbunge huyo alisema hayo wakati akiwahutubia wapigakura wake katika mikutano mbalimbali ya hadhara anayoifanya jimboni humo kuhamasisha shughuli za maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Alionya kuwa hali hiyo inawafanya wanachama wa chama hicho na wananchi wengine kudhani kuwa mwenendo wa viongozi hao kutowajali watu ndiyo maelekezo ya chama jambo alilolieleza kuwa linasababisha watu kuichukia CCM na serikali yake.
“Tamaa ya fedha na uchu wa madaraka ni sumu kubwa ndani ya chama hiki, wenye fedha wameingia madarakani kwa ajili ya malengo yao, mengi mazuri yanayofanywa na serikali hawataki kuyazungumza , kazi yao ni majungu, fitina na uongo na wamewasahau wananchi” alionya Ngonyani.
Aidha aliwataka wananchi kutochanganya urafiki ama itikadi katika masuala ya maendeleo na kwamba CCM siyo mbaya lakini baadhi ya viongozi ndiyo tatizo na chimbuko la watu wanaokichukia chama hicho na kudiriki hata kukihama na kuhimiza upendo, umoja na mshikamano ili kuondoa dosari zenye kukichafua chama hicho.
Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Wilayani Korogwe, Shebila Idd alieleza kuwa kiongozi anayetosha ni yule mwenye kubaini udhaifu na utendaji wa mwenye mamlaka na kutafuta ufumbuzi na kwamba asiwe wa kuzungumza upungufu wa mtu huyo kwenye vijiwe ambavyo vina watu wa itikadi tofauti .
Idd diwani wa kata ya Kerenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini, aliwataka viongozi kuonyesha njia na kwamba Watanzania watawapima kutokana na matendo yao.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment