KAMATI inayosimamia migogoro ya ardhi na viwanja katika eneo la
Kange Kasera jijini Tanga imevunja nyumba mbili zilizojengwa kinyume
cha utaratibu na wavamizi waliovamia bila ya kufuata utaratibu.
Zoezi hilo ambalo limesimamiwa na Ofisa Tarafa ya Pongwe, Juma
Msagati, umefanyika baada ya kamati hiyo kutoa taarifa ya kuvamiwa eneo
la viwanja ambalo bado lina mgogoro na kuanza kujengwa isivyo halali.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi hilo,
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dickson Mhando, alisema kuwa wamefikia hatua
hiyo baada ya wahusika kwenye viwanja vya wamiliki wengine pasipo
kufuata taratibu.
“Eneo la Kange Kasera lipo kwenye mgogoro wa viwanja, lakini upo
katika hatua za mwisho za kupata ufumbuzi sasa kuna watu wameanza
kuvamia maeneo na kujenga bila kufuata taratibu wakati eneo bado lina
mgogoro, hivyo tumeamua kuvunja,” alisema Mhando.
Alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kama kuna wavamizi
wengine wana nia kama hiyo waache hadi hapo utaratibu wa upimaji wa
maeneo utakapokamilika.
Hata hivyo, Msagati alisema kuwa kabla ya wavamizi hao kuchukuliwa
hatua za kubomolewa nyumba hizo, waliwataka wazivunje kwa hiari yao
kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa.
“Nilitoa taarifa kwa njia ya barua kusitisha ujenzi wa nyumba zao
kutokana na eneo wanalojenga kutokuwa mali yao, lakini walikataa
kufanya hivyo ndiyo maana tupo hapa na kamati kuvunja nyumba hizo
kutokana na kutoitikia wito,” alisema Msagati.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment