MAKOSA dhidi ya uhalifu wa kibinadamu katika Jiji la Tanga
yamepungua kwa asilimia 2.64 kwani kwa mwaka 2012 yaliripotiwa matukio
492 ukilinganisha na mwaka 2013 ambapo yalikuwa 479.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa jiji
hilo, Costantine Massawe alitoa taarifa ya hali ya uhalifu kwa kipindi
cha kuanzia Januari hadi Novemba 2013.
Kamanda Massawe aliyataja makosa hayo kwa mwaka huu ni mauaji 85,
kubaka 337, kutupa watoto 5, kulawiti 49 pamoja na wizi wa watoto 3
hali ambayo kwa mwaka 2012 ilikuwa tofauti.
Aliongeza kuwa mengine yalikuwa dhidi ya maadili ya jamii ambapo
jumla ya makosa 529 kwa mwaka 2013 yaliripotiwa ukilinganisha na 557
mwaka 2012.
“Katika kipindi cha mwaka huu ulioisha kulikuwa na ongezeko la makosa
ya kukutwa na bangi 196 yaliyoripotiwa ukilinganisha na mwaka 2012
ambapo yalikuwa 191, huku kosa la dawa za kulevya aina ya cocaine
lilikuwa moja,” alisema.
Alisema kuwa matukio ya ajali za barabarani yameongezeka ambapo kwa
mwaka uliopita matukio 28,334 ya ajali yaliripotiwa ukilinganisha na
mwaka 2012 ambapo yalikuwa 26,529.
“Makosa hayo yalisababisha vifo 105 ambapo wavulana walikuwa 83 na
wasichana 22, huku waliojeruhiwa kutokana na ajali hizo wakifikia 126,”
alisema.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo linawasaka watu 17 kwa kudaiwa
kuhusika na tukio la vurugu wilayani Kilindi pamoja na kuhusika na
vifaa vya milipuko katika Wilaya ya Handeni.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment