Mkoa wa Kilimanjaro pia umeonekana kuwa na dalili
za kuwa na madini ya urani na kuufanya mkoa huo wenye mlima mrefu kuliko
yote Afrika, kuwa na uwezekano wa kuwa na utajiri wenye manufaa makubwa
kwa Tanzania.
Wakuu wa mikoa hiyo, jana walithibitisha kuwa tafiti zilizofanyika kwa nyakati tofauti, zimethibitisha matumaini ya utajiri huo.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema
katika mkoa wake mafuta yamegundulika katika Bonde Pangani katika vijiji
vya wilaya za Moshi Vijijini, Mwanga na Same.
“Ni kweli kuna watu wanafanya utafiti wa mafuta
pale Chekereni Moshi Vijijini kuna mwelekeo wa kupatikana kwa mfuta
katika bonde lote hilo kuanzia Same hadi Moshi Vijijini,” alisema Gama.
Gama alisema ishara za kuwepo kwa mafuta ndizo zilizosukuma kuanza kwa utafiti huo.
“Tusubiri tuone yakipatikana itakuwa ni neema kwa Kilimanjaro na taifa,” alisema.
Wakati mkuu wa mkoa akisema hivyo, Mbunge wa
Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, naye
alithibitisha kuwepo kwa dalili za kupatikana kwa mafuta katika ukanda
huo.
“Ni kweli walianzia utafiti wao pale Ziwa Chala na
Ziwa Jipe halafu wakaenda hadi Kijiji cha Butu mpaka Mkomazi pale
jimboni kwangu na kuna dalili za kuwapo kwa mafuta,” alisema Profesa
Maghembe.
Profesa Maghembe alisema taarifa za wataalamu wa
miamba pia zinaonyesha kugunduliwa kwa madini ya Urani katika milima ya
Kijiji cha Kivisini.
“Hii ni neema kwa kweli kwa sababu rasilimali zote
hizi mbili zikigunduliwa hapa kwetu ni manufaa makubwa ya kiuchumi si
kwa mkoa tu lakini kwa taifa zima hili si jambo dogo,” alisema waziri.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alisema
dalili za kuwepo kwa mafuta katika ukanda wa bahari ya mkoa wake,
zimeanza kuonyesha matumaini na utafiti kwamba unatarajia kukamilika
mwaka ujao
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Gallawa alisema utafiti
huo unafanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Alisema mchakato wa utafiti bado unaendelea na
kwamba taarifa iliyowasilishwa serikalini inasema kuna dalili nzuri za
kupatikana kwa mafuta katika ukanda wa Bahari ya Hindi mkoani Tanga.
Aliwataka wananchi kusubiri taarifa rasmi kutoka TPDC iliyopewa mamlaka ya kutangaza kuwepo kwa mafuta.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment