Home » » Saba mbaroni wakidaiwa kutega mabomu

Saba mbaroni wakidaiwa kutega mabomu

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga,Constantine Massawe.
 
Jeshi la Polisi mkoani Tanga kwa kushirikiana na wakazi wa Kijiji cha Maili Kumi wilayani Korogwe, wamekamata watu saba kwa tuhuma za kuhusika kuweka mabomu yaliyokuwa yameandaliwa tayari kulipuka kwenye nyumba mbili tofauti za ibada.
Watuhumiwa hao ambao majina yao yanahifadhiwa, wanatuhumiwa kuhusika na kukutwa na vifaa mbalimbali vya kutengenezea milipuko ya mabomu pamoja na silaha za jadi ambazo pia zilikuwa zimefichwa katika nyumba hizo katika kijiji hicho.

Watu hao walikamatwa wakiwa na chupa 10 ambapo tano zilikuwa na  petroli zikiwa na tambi zake ndani, gololi 103 ambazo hutumiwa kwa milipuko, galoni kubwa mbili zilizokuwa na lita nne za petroli, majambia, mishale yenye sumu, soksi za kuzuia uso (mask) upinde, daftari lenye mafunzo ya kijeshi kuhusu namna ya kufungua na kufunga silaha.

Vifaa vingine ni mapanga,visu, mifuko ya sandarusi, manati, vifuniko 12 vya maji, kofia nne na vitambaa vya kufunga kichwani pamoja na tende walizokuwa wakitumia kama chakula.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alisema watu hao walikamatwa Desemba 17, mwaka saa 2:00 usiku wilayani Korogwe.

Alisema askari polisi wakiwa katika kizuizi cha Maili waliwatilia shaka vijana watatu waliokuwa wamebeba vifurushi na walipotaka wasimame walikimbilia msituni na ndipo mmoja alipokamatwa.

“Sasa baada ya kukamatwa huyu mmoja na ndipo alipopekuliwa na kukutwa na vifaa hivyo kwenye begi lake na msako wa kuwatafuta wengine ulipoanza,”alisema.

Hata hivyo, alisema katika msako huo ndipo walipobaini kuwapo kwa vifaa vingine katika nyumba mbili tofauti za ibada zilizopo kijijini hapo.
Alisema watuhumiwa hao baada ya mwenzao kukamatwa walikimbia kujificha kwenye nyumba hizo za ibada ndipo wakazi wa maeneo hayo walipowatilia mashaka na kutoa taarifa kwa polisi.

“Baada ya kukimbizwa wakaona mahali salama kwao ni kwenye nyumba za ibada, lakini wananchi wa eneo lile waliwatilia shaka na kuamua kutoa taarifa ndipo yalipokutwa hayo mabomu ambayo yalikuwa yameshaandaliwa kulipuka,” alifafanua Massawe.

Kwa mujibu wa Massawe, baada ya mahojiano ya polisi, watuhumiwa hao walibaini kuwa ni miongoni mwa waliokimbi katika operesheni ya kuwasaka wahalifu iliyofanyika mwishoni mwa Novemba mwaka wilayani Kilindi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa