Wakazi
wa Jiji la Tanga wametahadharishwa kuwepo kwa mchafuko wa bahari, hali
inayotokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya
Hindi na Visiwa vya Comoro.
Kufuatia hatua hiyo, wananchi wote hususan wavuvi na waogeleaji
baharini wanaagizwa kuchukua ahadhari kubwa ili kuepusha madhara
yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE, Mkuu wa Wilaya ya Tanga,
Halima Dendego, alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa walizozipata kutoka
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), hali hiyo itapelekea bahari
kuwa na mawimbi makubwa sambamba na upepo mkali.
Dendego alisema kuwa mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanataraji
kuukumba Mji wa Tanga kuanza juzi jioni hadi Desemba 26 leo, hivyo
wananchi wachukue tahadhari kwenye maeneo ya Pwani.
“Tunajua kuwa starehe yetu watu wa Tanga ni kutembea katika fukwe
na wengine kuogelea. Vilevile, shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi
hufanyika baharini hivyo natoa wito kwa wananchi kuchukuwa tahadhari na
kama inawezekana kutofika kabisa kwenye maeneo hayo,” alisema.
Nao baadhi ya wavuvi wakizungumza katika mahojiano na NIPASHE,
walisema kuwa mpaka sasa wapo baadhi ya wenzao ambao walienda baharini
na hawajarudi na hawana uhakika wa usalama wao kwani kumekuwa na
mchafuko mkubwa wa bahari.
“Ni kweli kumekuwa na mchafuko mkubwa sana wa bahari si unaliona
wimbi hilo linavyovuma na kuna wenzetu walienda baharini jana (juzi)
hatujui hatma yao,” alisema Mbaruku Jumaa.
Hata hivyo, walisema kuwa wameshatoa taarifa kwenye mamlaka husika
na kwamba hatua za ufuatiliaji zimeanza kuchukuliwa ili kubaini iwapo
kuna waliopata madhara kutokana na machafuko hayo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment