Home » » Mama mzazi wa Tido Mhando azikwa Tanga

Mama mzazi wa Tido Mhando azikwa Tanga

Muheza. Askofu mstaafu wa Anglikana Dayosisi ya Tanga, Phillip Baji ameongoza jopo la mapadri wa kanisa hilo mkoani Tanga katika maziko ya mama mzazi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya MwananchiCommunications Ltd, Tido Mhando, Jessie Nemganga Mhando (85) aliyezikwa katika makaburi ya Kanisa la Kristo Mfalme.
Baji aliongoza ibada hiyo juzi na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya waumini wa kanisa hilo, lililopo katika Kitongoji cha Mdaba Mjini Muheza na baadaye kwenye makaburi yaliyopo kwenye uwanja wa kanisa hilo.
Mapadri walioshiriki kuendesha ibada hiyo chini ya Baji, ni Cosmas Mhina, James Dominic, Christopher Kiango na Mchungaji Daniel Mhando ambaye ni baba mzazi wa Tido Mhando.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Baji aliwataka waumini wa dini hiyo kuiga mfano wa Jessie ambaye aliishi Kikristo katika maisha yake yote, akiwa kiongozi wa wanawake pamoja na jamii iliyomzunguka kwa jumla.
Katika salamu alizotoa mara baada ya mazishi, Mhando aliwashukuru waliojitokeza kuifariji familia hiyo na hasa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd ambayo ilibeba jukumu la kuushughulikia mwili wa marehemu tangu alipofariki Jumanne iliyopita.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa