Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Costantine Massawe
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika barabara kuu ya Segera - Chalinze eneo la Kwaluguru kata ya Kwedizinga Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wakati badi hilo likitoka Korogwe kwenda jijini Dar es Salaam.
Kamanda Massawe alisema ajali hiyo ilihusisha basi lenye namba za usajili T 610AGR aina ya Nissan lililokuwa likiendeshwa na Luta Mpenda (35), ambaye ni miongoni mwa waliokufa.
“Majeruhi wamekimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni ya Magunga na hali zao bado siyo nzuri na miili ya marehemu pia imehifadhiwa hapo," alisema Kamanda Massawe.
Hata hivyo, alisema chanzo cha ajali hiyo mwendo kasi uliomfanya dereva kushindwa kulimudu basi hilo.
Alisema majina ya watu waliokufa katika ajali hiyo hajatambuliwa na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Magunga.
Kamanda Massawe aliwaonya madereva kuacha mara moja tabia ya kuendesha mabasi kwa mwendo kasi ili kuepuka ajali kama hiyo ambayo imegharimu maisha ya watu hao wasio na hatia na wengine kuwaacha vilema.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo akizungumza kwa shida katika Hospitali ya Magunga alikolazwa, Francis Bendera, alisema awali basi hilo lilikuwa ligongane uso kwa uso na Fuso.
Hata hivyo, alisema dereva wa basi hilo alijaribu kulikwepa Fuso hilo lakini lilimshinda na kupinduka.
“Tukiwa tunakaribia kwenye kona, Fuso lilitupita kwa kasi sana na nusura ligongane uso kwa uso na basi tulilopanda lakini alijitahidi kukwepa. Hata hivyo, kutokana na kona ile kuwa kali, ndipo basi likamshinda na kupinduka,” alisema Bendera.
Nao baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walidai kuwa walisikia kishindo kikubwa katika eneo hilo na kwenda kuangalia kulikoni.
Walisema walipofika eneo la tukio, walikuta tayari baadhi ya abiria wamekwishafariki dunia.
“Tulikuwa tumekaa na ghafla tulisikia kishindo kikubwa na tulipokwenda kuangalia, tulilikuta basi la Burudan limepinduka...Kwa kweli ni ajali mbaya sana," aliliambia NIPASHE mmoja wa mashuhuda hao, Zablon Mbaga.
Wakazi wa Wilaya ya Korogwe walifurika katika hospitali ya Magunga kujaribu kutambua miili ya ndugu zao na baadhi ya majeruhi.
Aidha, baadhi ya wakazi wa Korogwe walisema basi hilo hupendelewa zaidi kupandwa na wafanyabiashara.
“Wengi ni wafanyabiashara ndiyo wanaotumia basi hili kwa kuwa na uhakika wa kuondoka hapa saa 12:00 alfajiri na kufika mapema Dar kisha kugeuza jioni," alisema Fatuma Bakari, mkazi wa wilayani Korogwe.
Basi hilo linadaiwa kubeba zaidi ya abiria 90.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Muzee Mungulwi, alisema majeruhi 12 ambao hali zao ni mbaya, wamekimbizwa katika hospitali mbalimbali zikiwamo Muhimbili jijini Dar es Salaam na KCMC mjini Moshi kwa matibabu zaidi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, alianza zoezi la uhamasihaji wa utoaji damu kwa wananchi ili kuwanusuru majeruhi hao ambao hali zao ni mbaya.
Akizungumza na NIPASHE, Gambo alisema kuwa majeruhi wengi wamepoteza damu nyingi hivyo mahitaji ya damu yamekuwa makubwa ukilinganisha na akiba iliyopo hospitalini hapo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment