Home » » WATUMISHI 7 WAFUKUZWA NA MADIWANI

WATUMISHI 7 WAFUKUZWA NA MADIWANI

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, limewafukuza kazi watumishi saba akiwemo daktari, matabibu, Maofisa Watendaji Kata na Vijiji.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo, Athanas Michael alipewa karipio kali baada ya kushindwa kuwajibika pamoja na Ofisa Kilimo Kata ya Mkindi, Ahimidiwe Mmari.
Azimio la kuwafukuza kazi watendaji hao lilipitishwa katika kikao cha madiwani hao ambapo Diwani wa Kata ya Tunguli, Bw. Michael Bomphe, alisema jukumu lao ni kusimamia shughuli zote za maendeleo pamoja na nidhamu kwa watumishi.
Bw. Bomphe ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Nidhamu katika baraza hilo, aliwataja waliosimamishwa kazi kuwa ni
Mganga Kituo cha Afya Songe, Dkt. Amir Juya ambaye hakuwepo kazini bila taarifa na tabibu Rashid Mnkande ambaye hakuwepo kwenye kituo cha kazi Zahanati ya Saunyi, siku tano.
"Wengine ni tabibu Msaidizi Kituo cha Afya Songe, Joseph Dioniz ambaye hakuwepo kazini kuanzia Januari mosi mwaka huu hadi Aprili na Ofisa Mtendaji Kata ya Negero, Confesi Mahimbo aliyeshindwa kusimamia shughuli za maendeleo na kuwaachia Maofisa Watendaji wa vijiji kuuza ardhi kiholela.
Aliwataja wengine kuwa ni Mtendaji wa Kijiji cha Lwande, Abdom Jaffu kwa utoro kuanzia Juni 6, 2012 hadi Julai mwaka huu, Cuthbert Kaale ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Negero, ambaye hakuwepo eneo la kazi siku tano na Ofisa Mtendaji Kijiji cha Mafulila, Piason Mhini aliyeshindwa majukumu.
Bw. Bomphe alisema Ofisa Mtendaji Kata ya Kwediboma, Bw. Mohamed Kimweri, aliyekuwa amesimamishwa alirudishwa kazini.

CHANZO MAJIRA

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa