Home »
» Halmashauri za mfano CHF kuzawadiwa
Halmashauri za mfano CHF kuzawadiwa
|
|
HALMASHAURI zitakazoandikisha kaya nyingi kuingia kwenye Mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF) zitazawadiwa kitaifa kutoka Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) imefahamika.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHIF,
Dk. Raphael Chegeni, wakati wa mkutano wa siku ya wadau mkoani Tanga
ulioitishwa na mfuko huo katika utaratibu wake wa kukutana na wadau
ngazi ya mkoa.
Dk. Chegeni alisema tayari menejimenti ya mfuko imeagizwa kuharakisha
mapendekezo hayo ili yawasilishwe kwenye bodi kwa uamuzi.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, hatua hiyo itakaporidhiwa itachochea
matokeo makubwa kufikia lengo la afya bora kwa wote na kuleta hamasa
mpya katika utekelezaji wa huduma za CHF ngazi ya halmashauri.
Aidha, aliutaka uongozi wa NHIF kushirikisha wadau katika hatua
muhimu za matayarisho ya tuzo hiyo ili kuleta mvuto na matokeo bora.
Dk. Chegeni alishauri kwamba jopo litakalotafuta washindi litokane na wadau wenyewe.
Akipongeza hatua hiyo, Maimuna Singano, ambaye ni mdau wa afya mkoani
hapa alitaka wigo uongezwe kwa kuwa wapo watendaji wa kata na vijiji
wanaofanya kazi ya kuhamasisha wananchi kuhusu CHF lakini juhudi zao
hazijatambuliwa.
Naye Mkurugenzi wa tathmini ya uhai wa NHIF, Michael Mhando alizitaja
halmashauri zinazofanya vizuri katika usimamizi wa huduma za CHF ni
Iramba, Singida Vijijini, Meru, Rombo, Igunga na zote za Mkoa wa Tanga.
Mara ya mwisho NHIF kutoa tuzo ilikuwa mwaka 2012 ambapo baadhi ya
halmashauri na mashujaa 50 wa mfuko huo wakiwemo waandishi wa habari
walitunukiwa tuzo hizo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati mfuko huo
ulipoadhimisha miaka 10 ya kuasisiwa kwake.
Chanzo;Tanzania daima
|
|
0 comments:
Post a Comment