WAFANYAKAZI zaidi ya 500 wa kiwanda cha nguo
Afritex Limited, mkoani hapa, wamegoma kufanya kazi hadi mkuu wa idara
kiwandani hapo atakapofukuzwa kazi.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, wafanyakazi
hao walisema hawamtaki mkuu huyo wa idara, Uchit Jha, kwa madai amekuwa
akiwanyanyasa kwa kuwatolea lugha chafu.
Mmoja wa wafanyakazi hao, Ferouz Hussein, alisema
Jha amekuwa pia akiwakata mishahara bila sababu, hivyo kuwasababishia kutofanya
kazi kwa uhuru na amani.
Naye Halima Juma alisema unyanyasaji unaofanywa na
mkuu huyo wa idara umekuwa ukizidi kila kukicha, hivyo kumtaka meneja wa kiwanda
hicho kumfukuza kazi.
Rajabu Mgaya alisema kuwa si kwamba wamegomea kazi
bali wamegoma kufanya kazi na mkuu wa idara huyo ambaye aliwahi kufanya kazi
kiwanda cha KTM Dar es Salaam na kufukuzwa kwa vitendo vyake vya unyanyasaji
kwa wafanyakazi.
Meneja wa kiwanda hicho, Prakash Kunnur, alisema
hajayapata malalamiko hayo na kwamba yakimfikia atayafanyia kazi ili kuondoa
mgogoro uliopo.
“Kwa sasa siwezi kujua kama malalamiko hayo hayana
ukweli au la kwa kuwa sijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wafanyakazi ila
nitalifanyia kazi na mambo haya hayatajirudia tena,” alisema Kunnur.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment