WAKAZI wa Kata ya Mbuzee, wanamtuhumu Diwani wao,
Rashid Shewedi (CCM), kuhujumu miundombinu ya maji na kujipatia kipato.
Wakizungumza na Tanzania Daima baadhi ya wanakijiji
walisema wamekuwa wakikosa maji safi na salama huku maji hayo yakiwanufaisha
watu wachache, akiwamo diwani huyo, anayeyatumia kwa kuyauza.
“Tanki ka maji la kijiji halina uwezo wa kugawa maji
kwenye mikondo mingi, lakini diwani ameruhusu mikondo zaidi ya 70 ambayo maji
yake yanakwenda huko kwa masilahi yake binafsi na sisi wananchi kukosa maji
hayo na badala yake tunayafuata umbali mrefu,” alisema Ahmed Shemela.
Wanakijiji hao waliongeza kuwa licha ya kuyafuata
umbali mrefu, maji hayo si salama.
“Maji tunayotumia ni ya Mto Soni, nayo si salama,
vinyesi vya chooni vinaingia humo na tunatumia muda mwingi kuyafuata,”
walisema.
Akizungumzia tuhuma hizo, diwani huyo alikiri
kuwapo kwa tatizo la maji kwenye kata yake na kukana tuhuma zilizoelekezwa
kwake.
Katika maelezo yake Shewedi alidai kuwa tatizo hilo
ni kubwa na si kijiji kimoja, bali karibu vijiji vyote hivyo wapo mbioni
kukarabati miundombinu.
“Mimi nasimamia miradi mikubwa ndani ya Halmashauri
ya Bumbuli, iweje ni hujumu maji kwa wananchi wangu?” alihoji na kubainisha
kuwa tayari wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji safi
na salama kwa vipindi vitatu kwa wiki.
“Hiyo mikondo 72 wanayolalamikia kuwa inaenda kwa
watu wengine kwa shughuli zao za kufyatulia matofali si kweli, kwa kawaida
galoni (tenki) lililopo linazalisha lita 20,000 kwa kutwa na kupelekwa mara
mbili kila kijiji, hivyo sasa ni wakati wa pamoja wananchi kujitokeza
kusaidiana na si kulalamika na kuingiza ushabiki wa kisiasa,” alisema.
Chanzo: Tanzania
Daima
0 comments:
Post a Comment