SHIRIKA la Viwango Tanzania {TBS} limefungia viwanda viwili mkoani hapa
kwa tuhuma za kuzalisha bidhaa zilizo chini ya viwango.
Viwanda hivyo ni Akiis Bonny (Top Tang) kinachozalisha bidhaa za Tomato
Sauce, Chilli Sauce na Bonny Cola, na kiwanda cha chumvi cha Hussein Salt
Works.
Akifungia kampuni hizo, mkaguzi mkuu kutoka makao makuu ya TBS jijini
Dar es Salaam, Hamisi Soudi alisema kuwa wamefungia uzalishaji bidhaa hizo
baada ya kubainika kuwa hazijathibitishwa na shirika hilo la viwango.
“Tunafungia bidhaa hizi mpaka pale watakapoleta kwetu na kuzithibitisha
kwa sababu huwezi kuwalisha watu bidhaa ambazo hazijathibitishwa,” alisema.
Soudi amewataka wakazi wa jiji la Tanga kuwa makini na bidhaa
zinazozalishwa viwandani, kwamba zikiwa hazina lebo ya TBS wanapaswa kuacha
kuzitumia kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima.
Mwanasheria wa TBS, Baptister Bitaho alisema kuwa mzalishaji yeyote bila
kujali ukubwa ama udogo wa bidhaa anayozalisha, anatakiwa apate nembo ya
TBS.
“Sisi hatujali kama ni mzalishaji mdogo au mkubwa, lazima kila
mmoja tumpatie nembo ya TBS kuthibitisha ubora wake,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment