Home » » WAZIRI MKUU PINDA KUFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA UWEKEZAJI KANDA YA KASKAZINI MKOANI TANGA

WAZIRI MKUU PINDA KUFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA UWEKEZAJI KANDA YA KASKAZINI MKOANI TANGA

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.


Na Dotto Mwaibale, Tanga

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda leo anatarajia kufungua mkutano wa kimataifa wa uwekezaji Kanda ya Kaskazini utakaofanyika mkoani hapa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Mkuu wa Mkoa huo Luteni mstaafu Chiku Gallawa alisema mkutano huo wa siku mbili utakaofanyika leo na kesho utatoa fursa ya kukuza uchumi wa mkoa wa Tanga.

“Mkutano huu utahudhuriwa na wawakilishi wa nchi zote zenye balozi hapa nchini na utafanyika Hoteli ya Mkonge mjini hapa” alisema Gallawa.

Alitaja mikoa iliyopo katika kanda hiyo itayoshiriki mkutano huo kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga ambao ni mwenyeji.
Alisema mkutano huo utatoa nafasi ya wananchi kuzitambua fursa zilizopo ambazo hazijafahamika vizuri kupitia wawekezaji hao.

Alisema maandalizi yote ya kuzitambua fursa zilizopo mkoani humo tayari yamefanyika na zitawekwa wazi katika mkutano huo ili kila mwananchi azielewe.

Alisema kuna fursa nyingi ambazo zinahitajika uwekezaji kwa ajili ya kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga na nchi ambapo alizitaja kuwa ni sekta ya kilimo, madini, ufugaji ambako kuna maeneo mengi ya malisho kama wilayani Handeni kwenye mashamba ya malisho 10 na Korogwe ambako kuna madini ya Jimsam yanayotumika kutengenezea chaki, unga wa kufungia mtu aliyevunjika ‘POP’ , chokaa na saruji ambayo yapo Kata ya Mkomazi.

“Wenzetu kutoka nje wana utalaamu na fedha na sisi tuna ardhi, rasilimali, miundombinu mizuri kama umeme na barabara hivyo ni vema kuchangamikia fursa hizo” alisema Gallawa.

Alisema katika mkutano huo kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazozarishwa na viwanda vilivyopo Tanga na zile za asili zinazotengenezwa na wenyeji wa mkoa huo.

Gallawa amewaomba wananchi wa mkoa wa Tanga kupitia vyombo vya habari kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano na kumpokea Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakayekuwa mgeni rasmi.

Alisema maandalizi yote kuhusu mkutano huo yamekamilika kwa kushirikiana na Halmsahauri zote za wilaya za mkoa huo.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa