na Mwandishi wetu, Tanga
WAKALA wa
Vipimo (WMA), wamebaini udanganyifu katika kituo cha mafuta cha WOCO wakati
wakifunga pampu za vipimo sahihi vya kuuzia mafuta mjini Korogwe mkoani Tanga.
WMA ilifunga
pampu mbili za petroli katika kituo hicho baada ya kubaini kuwa pampu hizo
zilikuwa zikiwapunja wateja kwa wastani wa mililita 150 hadi 200 katika kila
lita kumi.
Meneja wa WMA,
Mkoa wa Tanga, Lucas Mosha, alisema walibaini udanganyifu huo hivi karibuni
wakati wa ukaguzi wa kawaida ukiendelea ambao hufanya kila mwaka.
“Tuliwapa
taarifa kwamba tunaenda kukagua pampu zao lakini siku tuliyofika hakukuwa na
dizeli hivyo tukapima pampu za petroli tu, tulipofungua tukakuta ‘seal’ ya
serikali imekatwa, jambo linaloashiria kuchezewa kwa pampu hizo ili ziweze
kuwaibia wateja. Tulizifunga na kuwaamuru wasitumie pampu hizo hadi
watakapopata maagizo mengine.
“Tulipoondoka
tu, akaja mmiliki wa kile kituo akatoa zile lakiri tulizokuwa tumeweka na
akaondoa tangazo huku akitoa vitisho na tulipoona hali hiyo, tuliamua kutoa
taarifa polisi kwa ajili ya usalama,” alisema.
Mosha alisema
tayari ameiarifu WMA Makao Makuu kwa hatua zaidi za kisheria dhidi ya mtu huyo
kwani amekataa kukiri kosa na kutoa vitisho kwa watumishi wa mamlaka hiyo
waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment