Home » » WAZIRI APINGA UJENZI WA BANDARI YA MWAMBANI

WAZIRI APINGA UJENZI WA BANDARI YA MWAMBANI

Na Sussan Uhinga, Tanga
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, ameushauri uongozi wa Mamlaka ya Bandari, kuchukua hatua za haraka kuboresha bandari ya Tanga, ili kukabiliana na upinzani wa kibiashara.

Tizeba alisema, ni vema bandari hiyo ikaboreshwa, badala ya mkoa huo kutumia muda mwingi kufikiria ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani.

Ushauri huo aliutoa wakati alipotembelea bandari ya Tanga juzi, ambapo alisema kuwa suala la ujenzi wa bandari mpya ni la muda mrefu na utekelezaji wake umeonekana kuwa mgumu.

Dk. Tizeba alisema, ni vema bandari iliyopo ikaboreshwa, ili iweze kuleta faida kubwa kiuchumi badala ya kujenga bandari nyingine mpya.

"Jamani chukueni hatua za haraka za kuboresha bandari ya Tanga, ili iweze kuwa na tija pamoja na kuleta maendeleo ya haraka kwa jamii na mkoa kwa ujumla," alisema.

Dk. Tizeba alisema kuwa, bandari hiyo ya Mwambani, ilianza kufikiriwa kujengwa miaka mingi iliyopita na mpaka sasa ujenzi wake haujapata mafanikio yoyote.

Alishauri bandari iliyopo hivi sasa iboreshwe, ili iweze kupata wawekezaji wengi na soko kubwa kuongeza kipato katika nchi yetu na taifa kwa ujumla.

Naibu waziri huyo aliwataka viongozi wa bandari watambue ushindani uliopo sasa kwa nchi jirani, hivyo akasema kuwa huu sio wakati wa kupanga mikakati ya muda mrefu isiyo kuwa na utekelezaji.

Aliutaka uongozi wa bandari mkoani hapa, kuimarisha ulinzi wa bandari ili kuepuka dosari ambazo zinazoweza kujitokeza katika bandari hiyo ikiwamo wizi na upotevu wa mizigo ya wateja.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa