Na Amina Omari, Muheza
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Mbaramo wilayani
Muheza, wamesema kuwa shule hiyo imeshuka kiwango cha taaluma kutokana na shida
ya maji pamoja na uhaba wa vitabu vya kiada.
Hayo yalisemwa na wanafunzi hao wakati wakimweleza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Muheza, Ibrahimu Matovu, katika risala yao kwenye mahafali ya
kuhitimu kidato cha nne yaliyofanyika jana shuleni hapo.
Jamali Bakari wa kidato cha nne akisoma risala hiyo, alisema kuwa shule hiyo
inakabiliwa na shida ya maji na hivyo wanafunzi kutumia muda mwingi kutafuta
maji badala ya kusoma.
Alisema kuwa tatizo jingine ni upungufu wa vifaa vya kufundishia , maktaba ,
maabara na usafiri hivyo wanafunzi wamekuwa wakisoma kwa tabu kutokana na wengi
wao kuishi mbali na shule hiyo.
Wameiomba Serikali kuhakikisha wanatatua matatizo hayo kwa kuhakikisha
vinapatikana vitu hivyo kwa kuwa ndiyo muhimu kwa misingi ya elimu bora.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Sakwela alisema kuwa matatizo hayo yameanza
kushugulikiwa kutoka katika michango ya ada pamoja ya ujenzi wa shule hiyo na
kwamba kuna baadhi ya mafanikio yamepatikana katika shule hiyo.
Akijibu Risala hiyo, Mkurungezi wa Wilaya ya Muheza, Ibrahimu Matovu alisema
halmashauri ya wilaya hiyo itahakikisha inatatua tatizo la maji katika kipindi
kifupi kijacho.
"Matatizo mengine tutaendelea kuyatatua kwa kiasi fedha zinavyopatikana,
tutajaribu kumega fungu kidogo ili kuisaidia shule hiyo kwa nyakati tofauti
licha ya ufinyu wa bajeti uliopo sasa," alisema Matovu.
Kwa upande mwingine kuhusu nidhamu aliwataka viongozi wa shule hiyo kukaa na
wanafunzi hao ili kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa elimu na tabia njema.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment