Na Amina Omari, Korogwe
WATENDAJI wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe
wilayani hapa, wametakiwa kusimamia sheria ndogo ya kudhibiti uchafuzi wa
mazingira na kuwachukulia hatua wanaotupa taka hovyo ili kuhakikisha mji huo
unakuwa safi
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Peter Mabuga, wakati wa
kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Korogwe (DCC), kilichofanyika juzi
wilayani huo.
Alisema kuna udhaifu kwenye utekelezaji wa majukumu kwa baadhi ya watendaji wa
halmashauri, jambo linalosababisha mji huo kuwa mchafu.
"Ifike mahali kila mtu atekeleze majukumu yake pasipo kusukumwa wala
kuhimizwa, hasa suala la usafi, kwa nini sheria zimetungwa na Baraza la
Madiwani halafu hazitumiki, ni lazima sheria hizo zitumike ili kuboresha
mazingira ya mji huu kwa kuwalipisha faini wachafuzi wa mazingira,"
alisema Mabuga.
Naye Mkurungezi Halmashauri ya Korogwe Mjini, Lewis Kalinjuna alisema kwa sasa
halimashauri hiyo imeanza kusimamia kwa ukaribu usafi wa mji huo katika maeneo
ya katikati ya mji.
Alisema kinachofanyika sasa wananchi wanachangia Sh elfu moja kwa mwezi kwa
ajili ya kuzolewa taka katika mitaa yao na trekta ambalo limenunuliwa kwa fedha
za wananchi na halmashauri, huku wamiliki wakiwa ni wananchi.
Pia aliwataka viongozi kuwahimiza wananchi katika utunzaji wa mazingira na
uchangiaji wa uhuduma ya usafi wa mji huo kwa maendeleo ya mji.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment