Home » » WAFUNGWA GEREZA LA MAWENI WAGOMA KULA

WAFUNGWA GEREZA LA MAWENI WAGOMA KULA

Na Hellen Mwango
Wafungwa 31 wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaotumikia kifungo cha maisha na waliohukumiwa kunyongwa katika gereza la Maweni mkoani Tanga, wamegoma kula kwa siku tatu mfululizo kwa kile wanachodai kunyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi.

Wafungwa hao wanalalamikiwa mambo kadhaa ikiwemo kulishwa chakula kibovu na kuuziwa vyandarua vilivyotolewa bure na serikali na Mkuu wa gereza hilo, ASP Rajabu Mbilu.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na wafungwa hao na NIPASHE kuiona, mmoja wa maofisa waandamizi wa gereza hilo (jina tunalo), amekuwa akiwageuza vitega uchumi kwa kuwauzia vyandarua ambavyo vimetolewa bure na serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa Sh. 7,500 kila kimoja kwa kutumia fedha wanazozipata kutoka kwa ndugu zao wanaokwenda kuwatembelea gerezani hapo.

Katika barua ya wafungwa hao (majina na namba zao tumezihifadhi), imeeleza kwamba wafungwa 24 wanalala chumba kimoja, lakini kitu cha kushangaza ni kuwa ofisa huyo amewanyang’anya vyombo vya kulia chakula pamoja na ndoo za kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kuachiwa ndoo sita ambazo wanasema hazikidhi mahitaji yao.

Pia, wanadai kunyang’anywa televisheni ambayo wamenunuliwa na serikali pamoja redio ambavyo wanasema wana haki kisheria kuwa navyo kama wafungwa.

Kuhusu chakula, wanadai kuwa wanapikiwa maharage yaliyooza na ugali mchungu na kwamba wakilalamika hupewa adhabu ya kuvuliwa nguo na kupigwa virungu.

“Tumegoma kula leo (jana) siku ya tatu mpaka tupate haki zetu za msingi kama wafungwa. Hakuna vyombo vya kunawia maji wala kuwekea chakula, kuna hatari kubwa ya kupoteza maisha kwa kupata magonjwa ya mlipuko hapa gerezani… sisi ni wafungwa, lakini Rais Kikwete hajui kama (wanamtaja afisa huyo kwa jina), anatudhulumu huduma muhimu anazotupatia Rais wetu, hivyo tunagoma kula chakula chao,”  ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana saa 10 :25 alasiri, Kaimu Kamishna wa Jeshi la Magereza nchini, Fidels  Mboya, alisema hana taarifa kuhusu madai ya wafungwa hao, hivyo aliomba apewe muda wa kuzungumza na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kwa njia ya simu:

NIPASHE: Habari za Jumapili afande, kuna taarifa kwamba wafungwa 31 katika gereza la Maweni mkoani Tanga wamegoma kula siku ya tatu leo kwa sababu wananyanyaswa. Je,ni kweli?

Mboya: Sina taarifa, lakini naomba unipe muda niwasiliane na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga.

NIPASHE: Sawa. Je, nikupigie baada ya muda gani mkuu?

Mboya: Nitakupigia mimi mwenyewe nikishapata majibu sahihi.

Hata hivyo, alipopigiwa mara ya pili saa 11:09 alisema kwamba bado anasubiri taarifa kutoka kwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga.

“Bado nasubiri taarifa nitakupigia nikupe majibu sahihi,” alisema Mboya kwa njia ya simu.

Mwandishi alimpigia tena simu Mboya kufuatilia tukio hilo saa 12:15 jioni, lakini simu yake iliita zaidi ya mara tatu bila majibu.

Hivi karibuni, wafungwa wa gereza la Ilungu lililopo mkoani Mtwara, waligoma kula kwa siku kadhaa wakilalamikia chakula kibovu, kukatiwa huduma za matibabu pamoja na kupigwa na askari magereza.
Chanzo: Nipashe

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa