Home » » MEYA TANGA AKANUSHA KUUZA KISIWA

MEYA TANGA AKANUSHA KUUZA KISIWA


Na Mwandishi Wetu, Tanga
MEYA wa Jiji la Tanga, Omari Guled ameibuka na kukanusha madai ya kuhusishwa na uuzaji wa eneo la Kisiwa cha Mnyanjani kinachodaiwa kuuzwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga, kwa mwekezaji anayetaka kujenga hoteli ya kitalii eneo hilo.

Akizungumza na waaandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita Guled, alisema taarifa zilizoripotiwa katika vyombo vya habari, hazina ukweli kwani wakati wa harakati hizo yeye hakuwa diwani.

"Mwaka 2010 nilichaguliwa kuwa diwani wa kata ya Ngamiani Kaskazini, Desemba 29 nilichaguliwa kuwa Meya wa Jiji la Tanga na kazini nilianza kazi Januari Mosi 2011.

“...Sasa eti inaelezwa tangu mwaka 2007, Meya Guled, amekuwa akishirikiana na wawekezaji kwa lengo la kutaka kuwahamisha wananchi au mimi na diwani wa kata ya mzingani Mohamed Kombora, tumeshirikiana kuuza pia uwanja wa mpira, mimi wakati huo sikuwa Meya wa jiji hili,” alisema Guled.

Alisema kuwa, eneo linalolalamikiwa ni uwanja mdogo ambao unatumika kuchezea mpira wa miguu, ambao haupo katika eneo linalodaiwa ni kisiwa na kwa mujibu wa taarifa za Cipango miji namba 2/244/1291, eneo hilo lilitengwa kwa matumizi ya uwanja kwa ukubwa wa mita za mraba 6,300 (70c x90c).

"Eneo hilo limezungukwa na nyumba za makazi na mkondo wa bahari na eneo hili linamilikiwa kiasili, kwani hayajatwaliwa kwa mujibu wa sheria, hivyo halmashauri haina mamlaka kisheria kuuza au kumilikisha eneo hilo bila kupata ridhaa ya wamiliki wa asili, na ofisi yetu ya jiji haina kumbukumbu zozote za nani aliuziwa au kununua eneo hilo," alisema Guled.

Hata hivyo, alikiri kwamba, mgogoro uliopo ni kati ya wamiliki wa kiasili wa eneo hilo na jamii ambayo imekuwa ikiutumia uwanja huo kwa shughuli za michezo tangu mwaka 1966.

Meya Guled, alisema kamati ya maendeleo ya kata chini ya Mwenyekiti wake Fadhili Bwanga (CCM), ambaye ni diwani wa sasa badala ya Kombora, wamekuwa wakishughulikia ili kupata ufumbuzi wake na haujafika katika ngazi ya halmashauri.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa