na Bertha Mwambela, Pangani
WAKAZI wa
kijiji cha Saadani, kata ya Saadani, wilaya ya Pangani, mkoani Tanga,
wameilalamikia Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kushindwa kulipa fidia ya mali
zao zilizoharibiwa mapema mwezi huu na wanyama aina ya tembo kijijini hapo.
Akizungumza na
Tanzania Daima kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Odongo Abielo, alisema kumekuwa
na uharibifu mkubwa wa minazi zaidi ya 100 na nyumba 22 uliofanywa na tembo
kwenye makazi na mashamba yao.
Alisema mbali
na kupeleka taarifa kwenye ofisi za Hifadhi ya Taifa ya Saadani kuhusu
uharibifu huo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa ajili ya kuwalipa fidia.
“Tunasikitika
sana kuhusu hii hifadhi yetu hapa kijijini, kwani haitusaidii tunapovamiwa na
wanyama na kila tunapowafuata huwa hawachukui hatua yoyote,” alisema Abielo.
Kwa upande wake
mkuu wa hifadhi hiyo, Hassan Nguluma, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema
kuwa suala la fidia ni jukumu la wizara na si la hifadhi kwani wao bado
hawajapewa fungu kwa ajili ya matatizo ya fidia.
Alisema wao
pamoja na hifadhi zote nchini, tayari walishapeleka malalamiko hayo kwenye
wizara husika na kuwa swala hilo liko katika hatua za kushugulikiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment