Home » » KIWANDA CHAOMBA ARDHI YA KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI

KIWANDA CHAOMBA ARDHI YA KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI

Na Sussan Uhinga, Tanga
MKURUGENZI wa Kiwanda cha Neelkanth kinachotengeneza chokaa mkoani Tanga, Rashid Hamud, ameiomba Serikali kuwapatia eneo la ardhi hekta 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi.

Ombi hilo alilitoa mjini hapa jana kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Abdalah Kigoda, wakati alipokuwa katika ziara ya kutembelea viwanda.

Alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa kiwanda hicho zipatazo 120.

“Hapa tumezungukwa na maeneo makubwa ambayo yanamilikiwa na Amboni Estate, kwa kweli maeneo haya hayatumiki kwa kipindi kirefu zaidi ya miaka 50, tunaiomba Serikali itusaidie,” alisema Rashid.

Alisema kiwanda chake kina watumishi wa kudumu wapatao 425 na mkataba 600 ambapo jumla yake wanafikia 1,025 na ndio maana uongozi umeona kuna kila sababu ya kuwapatia makazi watumishi wao.

“Tunajivunia kuwekeza katika mkoa huu kwa kuwa tumefanikiwa kuboresha maisha ya wanajamii kwa kutoa nafasi za ajira na hatimaye na wao waweze kujikimu katika maisha yao,” alisema Rashid.

Akilitolea majibu suala hilo, Dk. Kigoda, alisema Serikali imesikia kilio hicho na kuwahakikishia wanakifanyia kazi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa