Home » » FUFUENI VIWANDA KURUDISHA HESHIMA YA TANGA: DK. KIGODA

FUFUENI VIWANDA KURUDISHA HESHIMA YA TANGA: DK. KIGODA

Na Gabriel Mushi, Tanga
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, amewataka wawekezaji katika sekta ya viwanda mkoani Tanga, kutimiza makubaliano kati yao na Serikali, kwa kuwezesha viwanda vyao kufanya kazi na kuzalisha bidhaa bora ili kuchangia pato la taifa.

Dk. Kigoda alitoa wito huo katika hitimisho la ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, iliyokuwa na lengo la kukagua viwanda na kuzungumza na wafanyabiashara wa mkoa huo, ili kuhimiza mkakati wa kufufua sekta ya viwanda na shughuli za biashara mkoani humo.

Katika ziara hiyo aliyotembelea viwanda mbalimbali, Dk. Kigoda alionyesha kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na mkoa huo katika kufufua viwanda vingi, vilivyokufa na kuanzisha viwanda vipya katika maeneo mbalimbali.

"Nawapongeza sana ndugu zangu wa Mkoa wa Tanga kwa juhudi kubwa nilizoziona. Nimefurahi kuona karibu kila kiwanda nilichotembelea kunamaendeleo makubwa, ajira zimeongezeka, bidhaa mnazozalisha zina ubora na viwango vya kimataifa.

“Katika hili, Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zenu kwa kuendelea kuimarisha miundo mbinu ya reli, barabara, bandari na upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme," alisema Dk. Kigoda.

Kwa upande wao, baadhi ya wenye viwanda na wafanyabiashara wa Mkoa waTanga, waliiomba Serikali kuangalia namna ya kuimarisha viwango vya kodi na ushuru mbalimbali wanaotozwa, ili waweze kumudu gharama za uzalishaji bila kuathiri ubora wa bidhaa zao.

Waliiomba pia Serikali kudhibiti wimbi la bidhaa zisizo na ubora zinazoingizwa nchini kutoka nje na kuuzwa kwa bei ya chini hali inayoathiri soko lao.

Akijibu hoja hizo, Waziri Kigoda alisema, anakerwa na tabia za urasimu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali, kwani hali hiyo inakwamisha jitihada za nchi kupiga hatua za kiuchumi.

“Wajibu wetu ni kuboresha mazingira ya kufanya kazi zenu, kuwaunga mkono na kuwasaidia kwa hali na mali, ili mtimize malengo na kamwe si kuwakwamisha," alisema Dk. Kigoda.

Aidha, Dk. Kigoda aliwataka wafanyabiashara hao kutumia fursa zilizopo katika Mkoa wa Tanga kwa kuzalisha zaidi, kusimamia viwango na ubora wa bidhaa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa