na Mwandishi wetu, Korogwe
MBUNGE wa Kinondoni, Idd Azzan, amekata mzizi wa fitina dhidi ya mahasimu wake kisiasa ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakieneza uzushi kwamba hajasoma na amelidanganya Bunge kuhusu elimu yake.
Mwishoni mwa wiki mbunge huyo alifanya ziara katika Shule ya Msingi aliyosoma ya Vuruni, Kata ya Chekeleni, wilayani Korogwe, mkoani Tanga ambayo wapinzani wake wamepata kueleza kwamba hajasoma katika shule hiyo.
Akiwa katika shule hiyo aliyosoma kuanzia mwaka 1973 hadi 1977 alipohamia jijini Dar es Salaam, mbunge huyo alikutana na mwalimu mkuu Mohamed Kombo na baadhi ya wanafunzi aliopata kusoma nao.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kombo alimshukuru mbunge huyo kuthamini mchango wa shule hiyo iliyofungua njia ya maisha yake.
“Ni mara chache sana kwa watu waliofanikiwa kisiasa na katika nyanja nyingine kutambua mchango wa shule zilizowatoa na kuzitembelea kama ulivyofanya Mheshimiwa mbunge. Kwa kuwa hili si jimbo lako, uamuzi wa kuja kututembelea ni jambo la kiungwana sana,” alisema Mwalimu Kombo.
Mwalimu huyo alieleza matatizo yanayoikabili shule hiyo kwa sasa, ni pamoja na uhaba wa vifaa vya michezo, milango kukosa vitasa pamoja na kukwama kwa ujenzi wa ofisi na stoo ya shule.
Kwa upande wake, Mbunge Idd Azzan aliahidi kugharamia ujenzi wa ofisi ya walimu na stoo kununua vifaa vya michezo, kufunga vitasa vya milango yote na matatizo mengine yanayoikabili shule hiyo.
“Hili si jimbo langu, lakini hii ni shule yangu kwani ndiyo niliyoanza kusoma, hivyo nawajibika kuisaidia kadiri ninavyoweza, kero ulizozitaja nitazigharimia kuziondoa,” alisema mbunge huyo.
Alimtaja mmoja wa watu aliosoma nao katika shule hiyo kuwa ni pamoja na Mhasibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Mhando na kuwataka na wengine kujitokeza kuisaidia shule hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment