Home » » DK. MWAKYEMBE ASHAURIWA KUKAGUA RELI YA TANGA

DK. MWAKYEMBE ASHAURIWA KUKAGUA RELI YA TANGA

Na Oscar Assenga, Tanga
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameshauriwa kufanya ziara za kutembelea reli ya Tanga na hatimaye aweze kujionea wizi wa mataruma, nguzo za simu na reli unaofanywa na baadhi ya wananchi.

Ushauri huo umetolewa na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Tanga Mjini, Khalid Rashid.

Alisema ni lazima Serikali ifanye ziara za kutembelea sehemu ambazo zimeathirika na wizi huo na kurudisha mifumo ya zamani.

Alisema wizi huo unafanyika sehemu mbalimbali mkoani hapa ikiwamo katika maeneo ya Genda genda wilayani Handeni karibu na Hifadhi ya Taifa ya Saadani na kusababishia hasara.

Alisema mfumo uliotumiwa hapo zamani ulikuwa mzuri uliokuwa hautoi mwanya wa kuibiwa miundombinu yake kutokana na kuwapo magenge katika njia za reli kila baada ya kilomita nane na wafanyakazi wa shirika hilo kufanya doria ya mara kwa mara kitendo ambacho hivi sasa hakifanyiki kila wakati.

Alisema njia za reli ziweze kuwa salama ni lazima kurudishwe mfumo wa zamani wa magenge uliokuwa ukitumika kama ulinzi katika maeneo ya reli na kuwapo na msisitizo wa awali wa wananchi kuziheshimu sheria za reli ikiwamo kuacha kupitia katika njia za reli.

“Chanzo cha uuzwaji wa vyuma chakavu unatokana na Serikali kuruhusu kuwapo kwa viwanda vya vyuma nchini bila kuwapo kwa upatikanaji wa malighafi hiyo,” alisema Rashid.

Alitoa wito kwa Serikali kutoa elimu kwa wananchi itayowawezesha kuwa mstari wa mbele katika kulinda miundombinu ya shirika hilo na kuongeza kasi ya mapambano.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa