Home » » MTOTO WA MIEZI SITA AOKOTWA JALALANI AKIWA AMEKUFA

MTOTO WA MIEZI SITA AOKOTWA JALALANI AKIWA AMEKUFA

Na Oscar Assenga, Tanga
MTOTO wa miezi sita ameokotwa jana asubuhi na wasafishaji wa eneo la kutupia takataka la Kwamama Nandala lililopo Mtaa wa Makorora, Kata ya Usagara akiwa ameshafariki dunia.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Commenti Centre B Makorora, Twahiru Ussi, alisema tukio hilo liligunduliwa na vijana wanaotafuta vyuma chakavu katika dampo hilo, ambapo wakati wakiendelea kutafuta waliona mfuko wa rambo uliokuwa umefungwa na kuamua kuufungua na ndipo walipokiona kichanga hicho kikiwa tayari kimekufa.

Alisema vijana hao walipofungua mfuko wa rambo hiyo wakiwa na mzee anayefanya usafi katika dampo hilo ndipo walipoamua kuwajulisha uongozi wa Serikali ya Mtaa na kufika eneo la tukio na kumuona mtoto huyo.

Alisema tukio hilo ni la kinyama na uzalilishaji na aliiomba Serikali iangalie namna ya kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaofanya vitendo hivyo.

Kwa upande wake, mkazi wa eneo hilo, Asha Juma, alisema tukio hilo ni baya katika jamii na alilitaka Jeshi la Polisi kumtafuta mwanamke aliyefanya tukio hilo na kumfikisha katika vyombo vya dola.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constatine Massawe, alisema hilo ni kosa la jinai na si maadili mazuri kwa dini zote na hata kwa jamii kwa wasichana kupata mimba na kuamua kuwatupa watoto wao.

Alitoa wito kwa wazazi kuacha tabia za kuwafukuza binti zao wanaopata ujauzito bila kutarajia, kwa kuwa kufanya hivyo kunasababisha matukio mengi ya kuokotwa watoto wachanga na kuwataka vijana wanaowapa mimba wasichana kutowakimbia.

“Wasichana wanaopata mimba waache tabia ya kuwaua watoto wanaowapata, badala yake wawazae na kuwapeleka katika vituo vya kulelea watoto kama wao watakuwa wameshindwa kuwalea watoto hao,” alisema Massawe.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa