Home » » KOROGWE WAHITAJI ELIMU YA UJASIRIAMALI

KOROGWE WAHITAJI ELIMU YA UJASIRIAMALI



Mwandishi Wetu, Korogwe
ASASI mbalimbali zinazojihusisha na utoaji elimu ya ujasiriamali nchini zimekaribishwa jimbo la Korogwe vijijini ili kutoa elimu juu ya mbinu zitakazoweza kusaidia kuwakwamua kiuchumi wananchi hasa vijana.

Wito huo ulitolewa juzi na mbunge wa jimbo hilo Stephen Ngonyani alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mamlaka ya mji mdogo wa Mombo.

Ngonyani anayefahamika zaidi kama Profesa Maji Marefu alitoa rai hiyo akisema kwamba ili kusukuma jitihada za maendeleo ya wananchi mbele atakuwa tayari kuziwezesha asasi zinazotoa elimu ya ujasiriamali ili wananchi  waweze kujikwamua kiuchumi.

"Mimi niseme kwamba niko tayari kusaidia gharama kwa taasisi ama asasi yeyote ambayo itakuwa tayari kuwasaidia wananchi wangu hasa vijana katika jitihada za kuwakwamua kiuchumi "alisema mbunge huyo.
Akizungumzia zaidi masuala ya vijana alisema iwapo wataonyesha utayari wa kujikwamua kiuchumi waendesha miradi yao ya kimaendeleo atatumia nafasi yake kuwasaidia ili waweze kupiga hatua za haraka.

Aidha alisema, hatakuwa tayari kuwasaidia wale ambao hawatakubali kubadilika kwa kuvunja sheria za nchi jambo ambalo ni kinyume na taratibu ambapo pia hata wakati mwingine maadili yanakataa.

Aliwahimiza vijana kuwa wabunifu na wanaopenda kujituma lengo likiwa kutafuta mbinu mbadala ya  kujikwamua kimaisiha huku akiwasihi kuepuka kukaa vijiweni na kujitumbukiza kwenye makundi maovu.

Wakati wote nitakuwa tayari kuwasaidia pale mtakaponyesha nia ya kufanya hivyo, ila naomba mjitume na muwe wabunifu kwani ninyi ndiyo nguvu kazi tunayoitegemea, sitopenda mnyanyasike "alisema Ngonyani.

Mbunge huyo aliwaeleza wananchi wa jimbo hilo la Korogwe vijijini kuwa bila kuchoka ataendeleza jitihada zake za kuhakikisha wanapata maendeleo akitumia mfuko wa jimbo na nguvu zake binafsi.

Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa