na Mbaruku Yusuph, Tanga
TIMU zaidi ya 30 zinatarajiwa kushiriki katika mashindano ya Kombe la Polisi maarufu kama Masawe Cup yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mapema mwezi ujao na kushirikisha wilaya zote za Mkoa wa Tanga.
Mratibu wa mashindano hayo, Sofia Wakati alisema lengo ni kujenga mahusiano mazuri kati ya polisi na raia kitu ambacho kinaleta tija katika ufanisi wa kazi za kipolisi na kuweza kufanikiwa kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kwa ushirikiano mzuri kati yao.
Alisema kwa sasa ipo haja ya kujenga urafiki mwema kati ya Jeshi la Polisi na raia kwa kupitia michezo na kuiondoa dhana mbaya ya uadui iliyojengeka muda mrefu na kulifanya jeshi hilo lishindwe kudhibiti vitendo vya uvunjwaji wa sheria kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa raia wema.
Sofia alisema kuwa maandalizi ya michuano hiyo yamekamilika, na alizitaja wilaya ambazo zitashiriki kuwa ni Pangani, Muheza, Korogwe, Lushoto, Handeni, Mkinga, Kilindi na Tanga Mjini.
Alisema kuwa kila wilaya itatoa timu moja ambayo itashiriki kumpata mshindi ambaye atashiriki mashindano ya mkoa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment