Home » » JELA MIAKA 25 KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA

JELA MIAKA 25 KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA

na Happiness Katabazi, Tanga
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tanga, imewahukumu kifungo cha miaka 25 jela washitakiwa sita ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu 92.2 na thamani ya sh bilioni 2.4.
Washitakiwa hao ni Kileo Bakari Kileo, Yahaya Makame, Mohammadal Gholamghader Pourdad, Salum Mparakasi, Said Hamisi na Bakari Kileo ‘Mambo’.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwaka wiki na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Kipenka Mussa ambapo alisema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na ushahidi ulitolewa na mashahidi 20 wa upande wa Jamhuri na vielelezo 25, na pia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa utetezi na vielelezo 15.
Jaji Kipenka alisema pamoja na kumhukumu kila mshitakiwa kwenda jela miaka 25, pia amewataka wailipe fidia serikali ya jumla ya sh bilioni 7.2 ikiwa ni mara tatu ya thamani ya dawa walizokamatwa nazo. Kwa maana hiyo, kila mshitakiwa atatakiwa kulipa sh bilioni 1.4.
Pia jaji aliamuru kielelezo cha 14 kilichotolewa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Biswalo Mganga ambacho ni magari mawili yaliyotumika kufanya uhalifu huo, serikali iyataifishe.
Itakumbukwa kuwa, mdogo wa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), Assad Aziz Abdulrasul alikuwa ni mshitakiwa katika kesi hii, lakini mapema Mei mwaka huu, jaji huyo alitoa uamuzi wake wa kumuachilia huru kwa maelezo kwamba hakuwa na kesi ya kujibu.
Awali ilidaiwa kuwa, washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Aprili Mosi na Machi 8 mwaka 2009 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, Tanga na Jamhuri ya Iran, walikula njama za kusafirisha dawa hizo.
Kosa la  pili ni ni la kukutwa na dawa hizo Machi 8 mwaka 2010 huko Kijiji cha Kabuku wilayani Handeni mkoani Tanga, kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa