Home » » MTENDAJI WA KIJIJI ATELEKEZA VIFAA VYA MBUNGE

MTENDAJI WA KIJIJI ATELEKEZA VIFAA VYA MBUNGE



Na Oscar Assenga, Korogwe


MBUNGE wa Jimbo la Korogwe, Stephen Ngonyani, ameshangazwa na hatua ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bungu, Mohamed Kalaghe, kushindwa kuvitumia vifaa vya ujenzi alivyotoa.

Vifaa hivyo vilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha polisi ili kutatua kero ya uchakavu wa kituo hicho katika tarafa ya Bungu, iliyodumu kwa muda mrefu.

Mbunge huyo aliyefika katika kijiji hicho akiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mrisho Gambo, alikagua jengo lililotolewa kwa ajili ya matumizi ya kituo cha polisi likiwa halijakarabatiwa.

Kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya kero hiyo, mbunge huyo alilazimika kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa lengo la kutatua kero hiyo.

Vifa alivyotoa mbunge huyo kupitia mfuko wa jimbo ni pamoja na mifuko 40 ya saruji, makopo ya mafuta ya rangi lita 40, nondo 20 za milimita 12 pamoja na Sh milioni 1.5 kwa ajili ya malipo ya fundi.

Katika hali ya kushangaza, mbunge huyo alikuta vifaa hivyo vikiwa havijafanyiwa kazi, licha ya kuvitoa tangu mwaka juzi kwa ajili ya ukarabati huo.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nifanye nini sasa, nimetoa vifaa hivi tangu mwaka 2010, lakini hadi leo vifaa hivi havijatumika, haya ni mambo ya kisiasa.

“Tunaleta maendeleo kwa wananchi, lakini wengine wana sababu zao wanaacha vifaa vinaharibika hapa, na hawa ndiyo watendaji wetu wa halmashauri,” alilalamika mbunge huyo.

Mbunge huyo alikuta ni sehemu moja tu ndiyo iliyojengwa ambapo fundi alitengeneza sehemu ya kuhifadhia silaha, lakini vifaa hivyo vyote vikiwa vimewekwa ndani ya jengo hilo.

Baada ya ukaguzi huo, mkuu wa wilaya aliwaamuru askari polisi alioongozana nao katika ziara hiyo kuwakamata mara moja mtendaji huyo pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mzee Mambo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, mbunge huyo alisema anahitaji ushirikiano na viongozi mbalimbali katika jimbo hilo ili aweze kutatua kero na ahadi alizozitoa wakati akigombea mwaka 2010.

Kwa upande wake mkuu huyo wa wilaya alisema atashirikiana na mbunge huyo kuhakikisha kwamba fedha anazotoa katika vijiji zinatumika.

“Wananchi wa Korogwe Vijijini mnataka mbunge wa aina gani tena, mbunge wenu tangu nimefika hapa nilipo sijawahi kuona mbunge wa aina hii,” alisema.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa